Kimataifa

Sudan Kusini yasema mwanahabari aliuawa kimakosa akiripoti mapigano

March 23rd, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

JUBA, SUDAN KUSINI

SUDAN  Kusini imesema uchunguzi wake kuhusu chanzo cha kifo cha mwanahabari Christopher Allen kilichotokea mwaka 2017 umebaini kuwa aliuawa katika tukio lisilokuwa la kukusudia katika ufyatulianaji wa risasi akiripoti matukio wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Allen aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ambaye alikuwa na uraia wa Amerika na Uingereza, alipigwa risasi kichwani wakati wa vita kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi katika mji wa Kaya, mnamo Agosti 26, 2027.

Sudan Kusini ilianza uchunguzi kuhusu kifo cha mwanahabari huyo mnamo Oktoba 2023 kufuatia shinikizo kutoka Amerika na Uingereza pamoja na makundi ya kutetea haki za wanahabari na haki za binadamu.

Awali, serikali ya nchi hiyo ilijiondolewa lawama kuhusu madai kuwa ilimuua Allen, ambaye alidaiwa kuegemea kundi la waasi wa Sudan People’s Liberation Army In Opposition (SPLA-IO).

Duru zilisema kuwa alikodiwa kuhudumia kundi hilo baada ya vita kulipuka nchini Sudan Kusini miaka miwili baada ya nchi hiyo kupata uhuru.

Mnamo Ijumaa, David Charles Ali Bilal, mkuu wa kamati ya kuchunguza kifo cha Allen, aliwaambia wanahabari kwamba “ilikuwa vigumu kubaini nani alikuwa mweupe na nani alikuwa mweusi” wakati wa makabiliano yaliyosababisha kifo cha mwanahabari huyo.

“Christopher Allen aliuawa kimakosa katika makabiliano ya risasi,” Bilal akasema akisoma ripoti hiyo.

“Allen aliingia Sudan Kusini kinyume cha sheria,” akasema akiongeza.

Pia alisema mwanahabari huyo hakuwa amevalia kinga yoyote wala mavazi ya kumtambua.

Watu 400,000 waliuawa katika vita hivyo vya 2013 hadi 2018 kati ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wa Riek Machar (sasa naibu wake).

Shirika la Wanahabari Wasiokuwa na Mipaka lilikuwa limeitaka Amerika kuongoza uchunguzi kuhusu kifo cha Allen, baada ya Sudan Kusini “kufeli kutambua wahusika.”