Kimataifa

SUDAN: Waandamanaji na jeshi kurejelea majadiliano

May 12th, 2019 2 min read

NA AFP

VIONGOZI wa waandamanaji nchini Sudan, jana walitangaza kwamba majadiliano yaliyokuwa yamesitishwa kati yao na viongozi wa kijeshi, yataendelea upya, mwezi mmoja tangu Rais Omar al-Bashir ang’atuliwe madarakani.

Muungano wa waandamanaji wa Alliance for Freedom and Change (AFC), Jumapili ulifichua kwamba umepata mwaliko wa kuanza upya mazungumzo kutoka kwa majenerali wa jeshi baada ya kusitishwa kwa siku kadhaa baada ya kukosa kuelewana.

Mwaliko huo ulitolewa huku mamia ya waandamanaji wakiendelea kukita kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, wakiapa kulazimisha jeshi kukabidhi mamlaka kwa raia jinsi walivyomlazimisha Bw Bashir kuondoka mamlakani.

“Tulipokea simu kutoka kwa Baraza la Jeshi ili tuendeleze upya mazungumzo yaliyokwama,” ikasema taarifa kutoka kwa muungano wa AFC

Mwezi uliopita, muungano wa AFC unaohusisha waratibu wa maandamano, vyama vya upinzani na makundi ya waasi ulipatia majenerali wa jeshi mapendekezo yao kuhusu namna ya kuunda serikali ya mpito inayoungwa mkono na raia.

Hata hivyo, majenerali hao walionekana kutopendezwa na baadhi ya hoja zilizokuwa kwenye mapendekezo hayo.

Majenerali walisema mapendekezo yaliyowasilishwa hayakugusia msimamo wa katiba kuhusu matumizi ya sheria ya Kiislamu maarufu kama Sharia ambayo ilikuwa msingi wa jinsi sheria nyinginezo zilivyotekelezwa chini ya utawala wa Bw Bashir.

“Tunataka kuandaa mazungumzo ya kina na kusuluhisha utata huu kwa muda wa saa 72,” ikasema AFC bila kutaja saa ambayo mazungumzo hayo yangeanza upya.

Hata hivyo, mamia ya waandamanaji ambao wanaendelea kutoa shinikizo kwa jeshi wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, wamesema lazima jeshi litoe mamlaka kwa wananchi wa Sudan.

“Tutakaa hapa milele hadi tupewe mamlaka,” akasema mwandamanaji Imam Hussein ambaye amekuwa kati ya waliokita kambi mbele ya makao makuu ya jeshi tangu Aprili 6.

“Wanatuchokoza na kufikiria tutakata tamaa lakini watashangaa. Tutazidi kukaa hapa tukifahamu mwishowe lazima tushinde,” akasema mwandamanaji mwengine kwa jina Hussein.

Kinaya hata hivyo ni kwamba ni waandamanaji wawa hawa waliokuwa wakitafuta msaada wa kijeshi ili kumtoa Bw Bashir uongozini na kusitisha utawala wake wa kidhalimu wa miaka 30.

Bw Bashir anayeendelea kuzuiliwa kwenye gereza la Kober alipinduliwa na wanajeshi Aprili 11 kisha baraza la kijeshi likatwaa mamlaka na kuahidi kuwapa raia mamlaka lakini hilo halijatimizwa hadi leo.