Habari MsetoSiasa

Sudi akaangwa kudai alilelewa Kikristo

July 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Kapseret Oscar Sudi amejisifu namna alilelewa vyema, akafunzwa maadili na Ukristo utotoni, malezi ambayo anadai yamemfaa na kumsaidia kuishi vyema.

Katika ujumbe ambao alituma kwenye akaunti yake ya Facebook Jumatatu, Bw Sudi, mbunge ambaye anafahamika kwa kutumia lugha chafu hadharani na kuwa kipau mbele katika vita vya kisiasa alisema alipokuwa kanisani akiwa mtoto, alifunzwa kupenda wengine, kutoa na kushukuru.

Mbunge huyo alichapisha picha zake na aliyemtaja kuwa mwalimu wake wa kanisani alipokuwa mtoto, huku akimshukuru vile alivyomlea vyema.

“Jana (Jumapili) nilitembelewa na aliyekuwa mwalimu wangu wa Sunday School Priscilla Tanui pamoja na mumewe Hoseah Tanui nyumbani kwangu Kapseret. Namshukuru kwa jukumu lake la kuhudumia jamii na jinsi alinilea kiroho.

“Alinifunza kutoa, kupenda na kushukuru. Tunafaa kujifunza kuwa tukishukuru wale ambao wamefanya mambo makubwa maishani mwetu,” akaandika mbunge huyo.

So wote waliochukulia ujumbe wa mbunge huyo kwa wepesi, hata hivyo, baadhi ya watu wakishangaa kwani wamemjua kwa kukabiliana na mahasimu wake kisiasa.

“Tunakujua kwa matusi, je ni yeye alikufunza hayo pia?” akauliza Korir CK, baada ya Bw Sudi kuandika ujumbe huo.

“Kulelewa kiroho ama nasoma nini, hiki ni kinaya,” akasema Kirongon Shadrack.