Sudi alitumia vyeti feki kuingia serikalini, mahakama yaambiwa

Sudi alitumia vyeti feki kuingia serikalini, mahakama yaambiwa

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA mkuu katika Taasisi ya Mafunzo ya Usimamizi almaarufu Kenya Institute of Management (KIM) sasa amefichua  kuwa mbunge  wa Kapseret Oscar Sudi alighushi cheti cha diploma cha msichana kutoka chuoni humo.

Bw John Kutima Matseshe anayesimamia masuala ya mitihani alisema cheti cha Diploma ambacho Bw Sudi alikabidhi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili kuidhinishwa awanie kiti cha Kapseret kilikuwa cha Bi Scholastica Achieng Odhiambo.

Bw Matseshe alieleza hakimu mkuu wa Mahakama ya Kuamua kesi za Ufisadi Bw Felix Kombo kwamba “nambari halisi ya usajili wa cheti hicho cha Diploma alichokuwa nacho Bw Sudi kilitolewa kwa Bi Odhiambo na wala  sio mwanasiasa huyo.”

Akiongozwa kutoa ushahidi na Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Riungu Gitonga, Bw Matseshe alisema Bw Sudi alighushi peupe cheti cha mwanafunzi aliyehitimu na Diploma katika Masuala ya Usimamizi wa Sekta ya Utalii.

Cheti hicho cha Bi Odhiambo ni nambari 20879 nacho kile Bw Sudi alikabidhi IEBC kilikuwa na nambari hiyo hiyo lakini cha taaluma ya “Usimamizi wa Masuala ya Ununuzi na Usambazaji.”

Bw Matseshe alisema alipelekewa nakala ya cheti hicho cha Diploma cha Bw Sudi na afisa wa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) kuthibitisha ikiwa kilikuwa halali.

“Nani alikupa cheti hiki cha Diploma cha Bw Sudi?” Bw Gitonga alimwuliza Bw Matseshe.

“Nilikabidhiwa cheti hicho na afisa wa EACC akitaka nithibitishe ikiwa Bw Sudi aliwahi somea mle KIM na ikiwa alihitimu kwa shahada Diploma,” alijibu Bw Matseshe.

Afisa huyo aliyesema licha ya kuwa siye anayehusika na kusajili wanafunzi wakijiunga na chuo hicho, cheti cha Bw Sudi cha Diploma kilikuwa ghushi.

Alisema alipekuapekua katika mitambo ya kompyuta yab KIM na kupata kwamba cheti cha Sudi hakikuwa halisi.

Bw Matseshe alifichua hayo alipotoa ushahidi katika kesi ambapo Bw Sudi ameshtakiwa kughushi vyeti vya kidato cha nne KCSE na Diploma.

Afisa mkuu wa kituo cha KIM John Matseshe akitoa ushahidi dhidi ya Sudi katika mahakama ya Nairobi Oktoba 27, 2021. Picha/RICHARD MUNGUTI

Bw Sudi amekanusha mashtaka tisa ya kughushi vyeti vya elimu na kuvikabidhi afisa wa IEBC Marine Mutali mnamo Januari 31 2013.

Mashtaka yanasema kuwa alitumia vyeti hivyo vya kughushi katika kaunti ya Uasin Gishu Bw Sudi pia ameshtakiwa kughushi cheti cha KCSE.

Afisa wa Baraza la Mitihani nchini,Bi Nabiki Kashu, alisema nambari ya cheti hicho cha cheti kilikuwa cha shule ya upili ya Parklands na wala sio cha Highway High School.

Mahakama ilifahamishwa jina la Bw Sudi halimo katika majina ya wanafunzi wa kidato cha nne waliotahiniwa na Knec.

Wakili Edwin Kiprono Chelugeti aliyepia chapa na sahihi Fomu za IEBC alizokabidhiwa Bw Sudi alimtambua kortini.

“Bw Sudi alikuja katika afisi zangu Uasin Gishu nimwidhinishie kwa kupiga chapa na sahihi Fomu za IEBC ndipo ateuliwe,” Bw Chelugeti alimweleza hakimu.

Bw Chelugeti alitambuliwa kwa hakimu kama yule aliyefika katika afisi yake kuidhinishiwa Fomu. Bw Sudi amekanusha mashtaka tisa ya kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na KIM.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 17, 2021 ili mshtakiwa asafiri hadi shule ya Upili ya Kabarak kumshughulikia mwanawe anayeugua.

  • Tags

You can share this post!

Raila ndiye baba wa ugatuzi, apewe urais 2022 – Junet

Bondia Ajowi kutetea hadhi ya Hit Squad

T L