Habari Mseto

Sukari nyingi nchini yashusha uagizaji kutoka nje

March 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

UAGIZAJI wa sukari ulishuka kwa asilimia 43 Januari 2018. Hii ni kutokana na kuwa bado kuna kiwango kikubwa cha sukari kilichoagizwa nchini wakati serikali iliondoa ushuru kwa sukari ya kuagizwa kutoka nje.

Kulingana na ripoti ya Afisi ya Sukari, kiwango cha sukari iliyoagizwa kilishuka hadi tani 38,829 Januari 2018.

Kenya iliagiza tani 900,000 kati ya Mei na Desemba mwaka 2017. Kiwango hicho kiliongezeka hasa baada ya serikali kuondoa ushuru kwa sukari ya kuagizwa Oktoba 2017.

Serikali ilitoa ushuru huo kwa sukari iliyoagizwa kutoka nje ya soko la COMESA.

Kulingana na afisi hiyo, idadi ya wanaoagiza sukari kutoka nje ya nchi imeenda chini, na ndio sababu kiwango cha sukari iliyoagizwa kimeshuka.

Hii ni kutokana na kuwa kuna sukari kiwango kikubwa nchini. Serikali ilichukua hatua hiyo mwaka uliopita baada ya uhaba mkubwa wa sukari kushuhudiwa nchini.

Hii ilitokana na ukame ulioathiri zao la miwa, na kuathiri uzalishaji wa sukari katika viwanda vya humu nchini.

Uhaba huo ulipelekea kupanda kwa bei ya bidhaa ya sukari nchini, ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh200.