HabariSiasa

'Sultan' aburudika majuu magenge yakihangaisha wakazi Mombasa

August 8th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

GAVANA Hassan Joho amejipata matatani kwa kukaa Amerika mwezi mmoja wakati kaunti yake inapokabiliwa na matatizo mengi.

Bw Joho, ambaye anatambuliwa kwa jina la utani la “Sultan”, alikashifiwa zaidi alipoonekana amepigwa picha akiwa na mwanamitindo Paris Hilton, siku ambayo majambazi walishambulia wakazi wa mitaa ya Bamburi Mwisho na Kwa Bulo na kuwajeruhi watu 13 vibaya.

Ofisi afisi yake iliandika taarifa ndogo na kuituma kwa vyombo vya habari akikashifu shambulizi hilo.

Bw Joho alielekea Amerika Julai 10 mara baada ya kukutana na Rais Kenyatta jijini Mombasa na kushuhudia Serikali Kuu ikikabidhi usimamizi wa egesho la pili la Bandari ya Mombasa kwa kampuni ya kigeni ya Mediterranean Shipping Company.

Shughuli hiyo ilisitishwa baadaye na mahakama hadi kesi iliyowasilishwa kupinga ubinafsishaji huo itakapoamuliwa.

Kulingana na msemaji wa Bw Joho, Richard Chacha, gavana huyo yuko Amerika kikazi na yeye kula starehe si kitu kigeni “kwani yeye pia ni binadamu”.

“Kile ambacho watu hawaelewi ni kuwa gavana pia ni binadamu kama mtu mwingine yoyote. Yeye yupo kazini na baada ya kazi lazima mtu afanye kitu ili aweze kupumzika,” Bw Chacha akaambia Taifa Leo.

Mwaka jana Gavana Joho alifanya ziara ya miezi miwili bara Asia na Uropa ambapo alizuru mataifa ya Ujerumani, Estonia na Dubai.

Tofauti na hapo awali ambapo Bw Joho alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya kiuchumi na kijamii ya wakazi wa Pwani, siku hizi amekuwa kimya wakati Serikali Kuu inapochukua hatua zinazohofiwa zitalemaza eneo hilo kiuchumi.

Alipokuwa ngangari kuwatetea wakazi wa Mombasa na Pwani kwa jumla, Bw Joho alisema bandari hiyo inapasa kuwa chini ya usimamizi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa, suala ambalo sasa liko mahakamani.

Wiki iliyopita Mamlaka ya Ushuru (KRA) na Mamlaka ya Bandari (KPA) ziliagiza mizigo yote iwe ikisafirishwa kwa reli ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Hatua hiyo, ambayo ingeanza kutekelezwa jana lakini ikasimamishwa Jumanne, inahofiwa itasababisha kufungwa kwa biashara nyingi na wafanyikazi kufutwa.

Licha ya athari za agizo hilo la KRA na KPA, Gavana Joho na ofisi yake walikuwa kimya, jambo ambalo awali angekuwa mstari wa mbele kupinga.

Ilichukua juhudi za wabunge Abdulswamad Nassir (Mvita), Badi Twalib (Jomvu) na Khatib Mwashetani (Lungalunga) pamoja na mashirika ya kijamii kushinikiza kusitishwa kwa agizo hilo.

Kulingana na wadokezi, kunyamaza kwa Bw Joho dhidi ya mpango wa masuala ya bandari ni kufutia uhusiano wake mwema na Rais Kenyatta baada ya mwafaka wa handisheki.

Akizungumza kabla ya kusafiri kwake, Bw Joho alisema: “Siku hizi wanauliza mbona nimenyamaza lakini kile ambacho mimi nawaambia ni kuwa siku hizi tumetoka katika ule wakati wa kushambuliana na sasa tunajadiliana iwapo kuna jambo lolote”.

Kabla ya mwafaka huo alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Kenyatta na alitumia kila fursa kumshambulia kiongozi wa nchi.

Ukakamavu huo wake wakati huo ulimfanya kupata umaarufu miongoni mwa wafuasi wa upinzani na alikuwa akishangiliwa kote alikoenda hasa katika ngome za ODM.

Huku Bw Joho akionekana kubadilisha mwelekeo mkali dhidi ya serikali, wachanganuzi wa siasa wameeleza kuwa nyota yake ya kisiasa imefifia.

Katika mahijiano na Taifa Leo, Profesa Hassan Mwakimako alisema kuwa kuinuka kisiasa kwa Bw Joho kulitokana na kupigania haki za wanyonge.

“Alikuwa anaonekana mshupavu na kuiweka serikali katika mtazamo kuwa inakadamiza haki zaa Wapwani. Jambo hilo halipo tena ndiposa watu wanaonekana kukosa imani naye,” akasema Profesa Mwakimako.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Joho, ambaye pia ni naibu kinara wa chama cha ODM alisema atawania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.