Suluhu asaidia kusuluhisha matatizo kati ya Wakenya na Watanzania

Suluhu asaidia kusuluhisha matatizo kati ya Wakenya na Watanzania

Na LEONARD ONYANGO

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta wamepata suluhu ya masaibu yaliyokumba uhusiano mwema kati ya mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki.

Hii ni kufuatia kipindi kirefu cha uhusiano baridi kati ya mataifa haya majirani.

Kufuatia mazungumzo yao Jumanne, Wakenya sasa wataenda kufanya biashara nchini Tanzania bila kuwekewa vikwazo mpakani.

Hii ni baada ya viongozi hao kuafikiana kwamba vikwazo visivyokuwa vya kodi viondolewe ili kuruhusu wafanyabiashara kupitisha bidhaa zao bila kuhangaishwa mpakani.

Mawaziri wa Afya wa Kenya na Tanzania nao watakutana kujadili namna ya kuhakikisha kuwa shughuli ya upimaji wa virusi vya corona mpakani inaharakishwa.

Baada ya kufanya majadiliano kwa karibu saa tatu katika Ikulu ya Nairobi, marais hao waliahidi kushirikiana katika masuala ya kibiashara, miundomsingi, usalama na utamaduni.

Pia walitia saini mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa.

“Gesi hiyo itatusaidia kupunguza gharama ya umeme na kulinda mazingira,” akasema Rais Kenyatta.

Waliwaagiza mawaziri wa Kenya na Tanzania kukutana mara kwa mara kutatua ‘matatizo madogo madogo’ yanayotatiza uhusiano kati ya mataifa haya.

Rais Kenyatta alisema waliafikiana na Rais Suluhu kuendeleza mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Malindi kupitia mpakani Lungalunga hadi Bagamoyo nchini Tanzania, pamoja na ufufuaji wa safari za majini katika Ziwa Victoria kati ya Kisumu, Bukoba, Mwanza na Jinja nchini Uganda.

Kiongozi wa Tanzania pia alitumia mkutano huo kumwalika Rais Kenyatta kuwa mgeni rasmi wakati kwa maadhimisho ya miaka 60 tangu Tanzania ilipopata uhuru wake Desemba 12.

Kenya ni ya tano katika kuwekeza nchini Tanzania, ambapo kampuni 513 za Kenya zimewekeza.

Kwa upande mwingine, kampuni 30 za Tanzania 30 zimewekeza nchini Kenya.

“Kuanzia sasa Watanzania tutakuja kuwekeza kwa nguvu zote hapa Kenya,” akasema Rais Suluhu.

Jumanne, shughuli ya usafiri katika Barabara ya Mombasa jijini Nairobi zilitatizika kwa saa kadhaa kufuatia msongamano mkubwa wa magari uliodumu kwa saa nne Rais Suluhu alipokuwa akielekea Ikulu.

Baadhi ya abiria ambao hawakutaka kuchelewa kazini asubuhi walilazimika kutumia bodaboda kuingia katikati mwa jiji na kutozwa nauli ya hadi Sh1,000.

Rais Suluhu pamoja na ujumbe wake waliposhuka kutoka katika ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Air Tanzania, saa 3.40 asubuhi, walikuwa wamevalia barakoa.

Lakini alipokuwa akiagwa na Makamu wa Rais Philip Mpango na viongozi wengine wakuu serikalini alipoondoka Tanzania, hawakuwa wamevalia barakoa.

Hiyo ni kawaida ya Rais Suluhu pamoja na ujumbe wake kuvalia barakoa anapozuru mataifa ya kigeni. Alivalia barakoa alipozuru Uganda Aprili 11, 2021.

Katika Ikulu, Rais Suluhu alilakiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kukagua gwaride la heshima na kupokea mizinga 21.

You can share this post!

Miaka yangu mitano kambini mwa Man-City sasa inaleta...

Urithi wa Raila wagawa ODM