Suluhu azima nyongeza ya ushuru, Wakenya wazidi kuumia

Suluhu azima nyongeza ya ushuru, Wakenya wazidi kuumia

Na PAUL OWERE

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameionya Mamlaka ya Ushuru (TRA), dhidi ya kupandisha ushuru.Rais Suluhu alisema mtindo huo ni wa kunyanyasa wafanyabiashara na raia, na badala yake akataka TRA itafute mbinu nyingine za kuongeza mapato ya nchi.

“Mmepatiwa kiwango cha TSh2 trilioni kwa mwezi. Nendeni mkapanue mbinu za kukusanya ushuru na kupata walipa ushuru wapya,” akasema rais.Uamuzi huo ni kinyume cha hapa Kenya ambapo ushuru wa kila aina umekuwa ukipandishwa kila uchao, hali ambayo imeongeza gharama ya maisha na kuporomosha biashara nyingi.

Rais huyo alikuwa akizungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwa katibu mpya wa Utumishi wa Umma, mawaziri na manaibu wao katika Ikulu ya Dodoma

.Kulingana na rais huyo, mtindo wa sasa unaua biashara badala ya kuimarisha mazingira ya kufanya biashara.“Mnatumia nguvu nyingi wakati wa kukusanya ushuru, sasa wale mnatoza ushuru mkubwa, mnatwaa vifaa vyao vya kazi, kufunga akaunti zao za benki, kwa sababu sheria inawaruhu kufanya hivyo, mnapofanya hivyo, wafanyabiashara wengi huamua kufunga biashara zao na kuhamia nchi nyingine,” alisema rais huyo.

Aliongeza: “Hii inapunguza idadi ya walipa ushuru. Kwa hivyo, ninawahimiza muende na kupanua ukusanyaji wa ushuru mkishughulikia masuala yanayofanya watu kutolipa ushuru.Alionya mawaziri dhidi ya kuketi na kutulia akisema Watanzania wanataka huduma na wanafaa kuwa nyanjani wakiwahudumia.

Awali, Makamu wa Rais Dkt Phillip Mpango ambaye pia alihutubu alisema bado kuna kazi nyingi ya kufanya katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya pesa za umma hasa katika serikali za wilaya, inayosimamia na Ummy Mwalimu.

Rais Samia ambaye alimrithi hayati John Magufuli wiki mbili zilizopita aliambia wanasiasa wanaomezea mate kiti hicho kusubiri. Alisema ni mapema kwa yeyote kutamani kuwa rais 2025 na akaonya kwamba atakuwa akiwatazama kwa makini. Rais hakutaja yeyote lakini aliashiria kwamba anafahamu kuna wanaoendeleza kampeni za mapema.

“Tafadhali zikomesheni,” alisema wakati wa kuapishwa kwa mawaziri wapya alioteua Jumatano akijipanga kuhudumu kama rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania.

Samia alikuwa makamu wa Magufuli kuanzia Novemba 2015 na aliapishwa rais baada ya mkubwa wake kufariki Machi 17, 2021.Kulingana na katiba, Rais Samia atamaliza kipindi kilichobakia cha zaidi ya miaka minne na ataweza kugombea kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Haikubainika mara moja kwa nini Rais Samia alitoa onyo hilo moja kwa moja kwenye runinga.“Ninajua kwamba kwenye kipindi cha pili cha urais Tanzania na pengine kwingine, wanasiasa wanang’ang’ania urithi lakini ninawaonya dhidi ya kampeni za mapema za uchaguzi wa 2025.”

You can share this post!

Akana kumlaghai mwenzake Sh36m

One Kenya Alliance ina mchongoma wa kupanda kisiasa