Habari

Sumu mitoni yatishia maisha ya mamilioni ya Wakenya

August 14th, 2019 2 min read

Na PAUL WAFULA

MAMILIONI ya Wakenya wanatumia maji na vyakula vyenye sumu kwao, wanyama na mazingira.

Katika muda wa miezi miwili iliyopita, Taifa Leo ilishirikiana na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa kufuatilia Mto Nairobi kutoka Kinamasi cha Ondiri katika Kaunti ya Kiambu, hadi Sabaki katika Kaunti ya Kilifi, ambako maji yake yanaingia Bahari Hindi.

Mto huo unapotiririka kuelekea Bahari Hindi unaungana na mito mingine ikiwemo Ngong, Athi River na Sabaki.

Katika kila hatua wanasayansi hao walichukua sampuli katika maeneo mbalimbali hadi Mto Sabaki. Kwa jumla sampuli 49 zilikusanywa katika maeneo ya Ondiri, Gikomba, 14 Falls, Dandora, Outer Ring, Ndwaru/Satellite, Thwake Dam na Sabaki.

Sampuli hizo zilikuwa ni pamoja na maji, samaki, mboga zinzokuzwa kwa maji ya mto huo zikiwemo sukuma wiki, kabeji, spinachi na managu.

Kisha sampuli hizo zilipelekwa Nairobi kufanyiwa ukaguzi wa maabara.

Uchunguzi wa wanasayansi uligundua jumla ya vyuma 12 na ikathibitishwa kuwa hakuna sehemu ya Mto Nairobi iliyo salama hata katika chemichemi yake Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na Prof James Mbaria, ambaye aliongoza wanasayansi hao, madini hatari zaidi yaliyogunduliwa ni mercury, lead, arsenic na cadmium kutokana na madhara yake kwa binadamu na wanyama.

“Madini haya ni sumu kwa binadamu. Hata ukichemsha chakula ama maji yenye madini haya ni kazi bure kwani hayaishi nguvu na lazima yatadhuru mwili wako,” aeleza Prof Mbaria.

Uchunguzi huo ulionyesha kuwa maeneo ambako sumu ya lead iko juu ni Kinamasi cha Ondiri, Chiromo, Gikomba, Dandora na Malindi.

Lead sawa na Mercury husababisha maradhi kama vile uhaba wa damu mwilini, kujihisi mnyonge, magonjwa ya figo, ubongo na hata kifo.

Madini ya selenium nayo yalipatikana kuwa ya kiwango cha juu. Yakiwa katika viwango vya chini, selenium inasaidia mwili kupunguza msongo wa mawazo na kuimarisha kinga kwa wanaougua Ukimwi, homa, kifua kikuu na hoya ya ini.

Lakini yakiwa ya kiwango cha juu, madini ya selenium husababisha upara, halufu mbaya, unyonge mwilini na kuharibika kwa neva.

Samaki, kaa na changarawe zilizochunguzwa pia zilipatikana kuwa na madini 10 hatari hasa chromium, arsenic, cadmium, lead, selenium, copper, aluminum, manganese, barium na chuma.

Kaa waliochukuliwa Malindi walikuwa na madini ya arsenic mara 38 zaidi ya kiasi kinachokubalika. Kulingana na Prof Mbaria, kiasi hicho kinasababisha maradhi hatari ikiwemo kansa.

Alisema kuwa kiasi hicho kikubwa kinatokana na uchafu kutoka viwandani.

Uchunguzi ulionyesha kuwa maji yaliyochukuliwa maeneo ya Chiromo, Gikomba, Dandora na Outer Ring yana kiasi kikubwa cha viini vya bakteria. Pia kulikuwa na kiasi kikubwa cha minyoo.

Uchafu wa viwandani nao ulionyesha kuwepo kwa madini hatari ingawa kwa kiwango cha chini.

Kulingana na wanasayansi, utumiaji wa maji chafu yaliyochanganyika na madini yenye sumu ni moja ya sababu za kuongezeka kwa magonjwa hatari nchini hasa kansa, figo, moyo na homa ya mapafu.

Mwaka jana pekee, Wakenya milioni 21 waliugua magonjwa ya kupumua, ambayo hasa husababishwa na madini.