Michezo

SUNDERLAND SAMBA FC: Mabinti wanaojitolea kukabili ukekeketaji Narok

May 26th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

SUNDERLAND Samba FC inayopatikana eneo la Mashangwa katika Wilaya ya Kilgoris, Kaunti ya Narok imeorodheshwa kati ya vikosi vinavyotumia mchezo wa soka ya wanawake kukabili masuala tofauti miongoni mwa jamii.

Sunderland Samba FC ya Kilgoris ilianzishwa mwaka 2005 na Maureen Auma ofisa kuu wa kikosi mwenza chenye makazi yake katika eneo la Kibera, jijini Nairobi.

”Nina timu mbili za wasichana, Sunderland Samba FC ya Kilgoris na Sunderland Samba ya Nairobi ambayo huu ni mwaka wa pili inashiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza,” alisema. Licha ya mawimbi kibao anaamini atakuza soka wasichana wengi sehemu hiyo.

Sunderland Samba FC ya Kilgoris inayojumuisha wachezaji ambao husomea katika shule ya Msingi ya Chamrecc, Narok hutumia soka kupigana na ukeketaji kwa wasichana eneo hilo.

”Kando na kukuza talanta hutumia mchezo wa soka kuhamasisha jamii kuhusu kudumisha amani baina ya jamii za maeneo hayo,” naibu wa kocha, Sayo Kindilupa alisema na kuongeza kuwa wao hupitia wakati mgumu maana jamii ya maeneo hayo inatambua zaidi mila na tamaduni zao.

”Kusema kweli hupata wakati mgumu kuelezea wazazi umuhimu wa kutowafanyia tohara wasichana ambapo wengi wao husema hata wakisoma hadi chuo kikuu tohara ni lazima kwa wanao,” alisema.

Kadhalika kocha huyo akishirikiana na mwenzake, Joel Muniko hutumia mpira kupata nafasi mwafaka kuwaelimisha wasichana hao jinsi ya kujidumu kimaisha baada ya kumaliza masomo. Naibu kocha huyo anasema vigoli wengi maeneo hayo wakishakamilisha shule mara nyingi huwazia kuolewa.

Katika kaunti ya Narok hakuna timu za michezo za kijamii maana wakazi wa maeneo hayo kamwe haitambui michezo.

Kwa kuzingatia sehemu hizo hakuna timu zingine za soka la wanawake, kwenye jitihada za kukuza talanta za mchezo huo Sunderland Samba hushiriki mechi za kirafiki dhidi ya vikosi vingine vya shule za msingi katika Kaunti hiyo.

”Hakika kwa muda huu wasichana wangu wamejaa motisha ambapo wamezamia mazoezi makali maana wiki watashiriki ngarambe ya siku moja itakayoshirikisha timu nne kutoka shule ambazo ni majirani zetu ,” kocha Muniko alidokeza kuwa mara nyingi, Sunderland Samba ya Kilgoris na Sunderland Samba ya Nairobi hutembeleana kusudi kucheza mechi za kupimana nguvu.

Mara kwa mara wachezaji wa Sunderland Samba Kilgoris hutembelea wenzao jijini Nairobi pia wenzao hao pia hutembea mjini Kilgoris.

Maureen anahimiza wasichana waliotuzwa kipaji cha kugaragaza boli kusaka timu za kujiunga nazo kwa ajili ya kuzichezea ili kupata nafasi mwafaka kunoa makucha yao katika kandanda.

”Sekta ya spoti imeibuka kitega uchumi kama ajira zingine duniani,” alisema. Anashauri kuwa wanaowazia kuibuka wachezaji tajika duniani wafahamu kuwa ni muhimu kudumisha nidhamu nyakati zote.