Michezo

Sunderland Samba walivyotwaa ubingwa

November 14th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Sunderland Samba ilibeba taji la Slum Champion na kuonyesha kwamba imepania mkuu kwenye kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu. Wasichana hao walipata kibarua kigumu mbele ya Lexus FC kabla ya kutwaa taji hilo kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali iliyopigiwa Uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Vipusa hao walivishwa ubingwa huo baada ya kushinda wenzao kwa kufunga magoli 5-4.

MAUREEN OSOSA

Kikosi hicho chini ya makocha, Joseph Odhiambo na Kelvin Baraka kilishuka dimbani kwa matamanio ya kulemaliza wapinzani wao ambao lakini shughuli ziliibuka moto. Ndani ya kipindi cha kwanza wasichana mnyakaji wa kikosi hicho, Maureen Ososa alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa mara kadhaa licha ya kubakia uso kwa macho (one on one) na mpinzani wake.

Kocha Odhiambo anasema “Bila shaka kipa wetu alifanya kazi nzuri licha ya kuonekana kulemewa na wapinzani wetu. Mchezaji tunampa hongera kwa jinsi alivyosaidia katika fainali hiyo hadi alipookoa mkwanju wa penalti.”

WALIOFANA

Kando na mnyakaji huyo bosi wa kikosi hicho, Maureen Obonyo alishukuru wachezaji wenzake watano waliofanya kweli katika fainali hiyo ikiwamo

Caren Awuor, Lorna Nyarinda, Jemin kahindi, Faith Kavinya na Angela Mirenje.

Naye naibu kocha Kelvin Baraka alisema kulingana na matokeo hayo wasichana hao wanaweza kufanya vizuri katika ligi msimu huu na kuzoa tiketi ya kupandishwa ngazi kucheza ligi kuu muhula ujao.

NUSU FAINALI

Kwenye nusu fainali Sunderland Samba ilidunga Santos FC bao 1-0 nayo Lexus FC ilivuna mabao 2-0 dhidi ya Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) ambayo hushiriki Ligi Kuu nchini (KWPL). Katika robo fainali, Sunderland Samba ilikomoa Raiders Queens mabao 2-0, KGSA ilizoa mabao 2-0 mbele ya Kibera Queens, Santos FC ilibeba idadi sawa na hiyo dhidi ya Kibera Angels nayo Lexus FC ilishinda Challengers mabao 5-4.

Mdhamini wa mashindano hayo, Yakub Jaffar alisema kwamba analenga kuendelea kuandaa kipute hicho kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wanasoka wengi tu wanaopatikana katika eneo la Kibera.

”Nimegundua kwamba Kibera ina wachezaji wengi wa michezo mbali mbali wanaohitaji kushikwa mkono ili kupapania vipaji vyao maana ndiyo wachezaji wa kimataifa wa kesho. Wengi wamepania kushiriki soka la kulipwa kama Doreen Nabwire aliyewahi kushiriki mchezo huo nchini Ujerumani miaka iliyopita.”