Michezo

Sunderland Samba yakomoa wapinzani

June 5th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WASICHANA wa Moving The Goalpost (MTG) wamerejea makwao huku wakinuna baada ya kudondosha alama sita muhimu walipojikuta hoi mbele ya Kahawa Queens na Sunderland samba kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza.

Sunderland Samba ilijiongezea alama sita na kurukia uongozi wa ngarambe hiyo ilipolaza Soccer Sisters mabao 3-0 kisha kukomoa MTG mabao 2-1 katika uwanja wa KNH, Nairobi. Vigoli wa MTG walikiri kichapo hicho huku wakiumiza jeraha la kuchomwa mabao 4-0 na Kahawa Queens inayokuja kwa kasi kwenye michezo ya kipute hicho msimu huu.

Hata hivyo ufanisi wa Sunderland Samba ambayo hutiwa makali na kocha, Joseph Odhiambo na Vince Baraka ulionyesha wazi kwamba kina dada hao wamepania kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Wasichana wa MTG walinasa alama sita kutokana na juhudi zao Elizabeth Mwajuma na Sylvia Akoth walipotikisa nyavu mara mbili kila mmoja naye Doreen Ingaitsa aliitingia bao moja.

”Napongeza wasichana wangu kwa kufanya kazi nzuri licha ya mvua kuwanyeshea uwanjani,” ofisa mkuu wa Sunderland, Maureen Auma alisema.

Nao Neddy Atieno, Lilian Shamala, Emily Auma na Everlyn Juma kila mmoja alipiga kombora moja safi na kusaidia Kahawa Queens kuzoa ufanisi wa tatu mfululizo na kutua katika nafasi ya nne bora kwa alama tisa.

Nayo Limuru Starlets ilinasa sare ya nne ilipotoka nguvu sawa mabao 2-2 na Mombasa Olympic huku Mukuru Talent Academy ikiendelea kusalia tatu bora ilipotwaa mabao 2-0 mbele ya Joylove FC.