Sunderland Samba yakubali yaishe Kangemi Starlets ikitesa

Sunderland Samba yakubali yaishe Kangemi Starlets ikitesa

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa timu ya kina dada ya Sunderland Samba, Joseph Ochieng amesema kuwa wanafikiria mipango ya kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza muhula ujao.

Amedokeza kuwa kwenye kampeni za msimu huu wana mechi moja kapuni lakini hata wakishinda hawawezi kupiku wapinzani wao Kangemi Starlets.

Jumapili akizungumza na Taifa Leo alisema, ”Hatuna lingine ila tumekubali yaishe wala sina budi kutaja kuwa kampeni za msimu huu kamwe hazikuwa mteremko.”

Sunderland Samba ambayo hushiriki mechi za Kundi A ilipoteza tumaini la kunasa taji la muhula huu ilipogongwa bao 1-0 na Kangemi Starlets mnamo Juni.

Kwenye patashika ya wikendi, Sunderland iliangusha Limuru Starlets ya kocha James Kairu kwa mabao 2-1.

“Mechi yetu dhidi ya Kangemi Starlets ilikuwa muhimu zaidi lakini tuliteleza na kudondosha pointi zote muhimu,” akasema.

Kwenye mechi nyingine, Soccer Sisters ilituzwa ushindi wa mezani baada wa wapinzani wao Mombasa Olympic ‘kuingia gizani’.

Nao vigoli wa Msato Starlets walishinda majirani zao MTG United kwa mabao 2-0.

Katika jedwali Sunderland inakamata nafasi ya pili kwa alama 25 kutokana na mechi 13 ambapo mchezo wa mwisho itakaribisha Msato Starlets katika uwanja wa NCC Ngong Road, Nairobi.

Msato Starlets inaburura mkia kwa kusajili alama tisa katika jedwali la timu nane.

Kangemi chini ya kocha, Joseph Orao ingali kifua mbele kwa kusajili alama 36 baada ya kushinda mechi zote 12 ambazo imeshiriki. Nafasi ya tatu imeshikiliwa na MTG United kwa alama 19, sawa na Soccer Sisters tofauti ikiwa idadi ya mabao.

You can share this post!

Muturi awarai vijana wasake vyeo vya uongozi

Pelico Jam na FC Talents zatoka sare ya 2-2