Kimataifa

Sungura 27 wahangaisha maafisa katika kituo cha treni

May 31st, 2018 1 min read

MASHIRIKA na VALENTINE OBARA

NEW YORK, AMERIKA

MAAFISA wa kutunza wanyama walikabiliwa na wakati mgumu kukamata sungura 27 waliotupwa katika kituo cha garimoshi cha Ronkonkoma, Kaunti ya Suffolk, Amerika.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, sungura hao walitupwa na watu wasiojulikana na haijulikani walikuwa na lengo gani.

Shirika la kutunza wanyama la Kaunti ya Suffolk lilinukuliwa kusema kwamba waliarifiwa kuhusu kisa hicho ambacho walikitaja kuwa cha kusikitisha kwani sungura hao hawajui kuishi katika mandhari ya nje kama hayo.

Shirika hilo liliahidi kutoa zawadi ya dola 3,500 (Sh350,000) kwa yeyote ambaye angewapasha habari kuhusu aliyetupa sungura hao.

Haikuwa rahisi kuwakamata sungura hao kwani walikuwa na hofu na kila wakati mtu alipowakaribia, walitoroka, kwa mujibu wa mashirika ya habari.

Ilibidi baadhi ya wakazi wajitolee kusaidia kwa hiari kuwakamata wanyama hao ili wapelekwe eneo salama kwani shughuli ya kuwakamata iliendelea hadi usiku.