Makala

Sunni Anjuman wanavyoinua maisha ya Waislamu maskini

March 10th, 2019 2 min read

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

CHAMA cha Waislamu wa Sunni Anjuman kimeimarisha jitihada zake za kuinua hali ya maisha ya wakazi wa ukanda wa Pwani.

Chama hicho kilianzishwa miaka ya 1980 kwa lengo ya kuwasaidia Waislamu wasiojiweza, na hasa mayatima.

Mwanzilishi wa chama hicho ambaye pia ni mwanachuoni mashuhuri, Almarhum Al-habib Ahmad Mash-hoor bin Twaha Al-Haddad ndiye pia aliweka jiwe la msingi la Msikiti wa Hidaya na Madrassa ya Darul-Ulum.

Almarhum Ustadh Mohammad Shariff Said Albeidh na Shariff Abdulkadir bin Mohammad Sayyid Abubakar bin Salim ndio waliotwikwa jukumu la kusimamia Madrassa hiyo ya Darul-Ulum. madrassa hiyo kwa sasa ina wanafunzi yatima wanaosoma na kulala hapo bila malipo yoyote.

Mwenyekiti wa Sunni Muslim Anjuman, Bw Mohammed Abdushakur alisema kwa wakati huu, madrassa hiyo ina jumla ya wanafunzi 120, ambapo 100 kati yao ni wanafunzi wanaopata mafunzo ya jioni ilhali 20 ni wale wanaosoma na kulala hapo.

Baadaye, chama hicho kilifanikiwa kujenga madrassa nyingine pamoja na msikiti unaojulikana kama Taqwa eneo la Mazeras. Madrassa hiyo ina wanafunzi 20, wote ambao ni mayatima wanaoishi mahali hapo.

Bw Abdushakur alisema chama hicho pia kinasaidia kutoa matibabu kwa jamii zisizojiweza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani.

Chama hicho kiliwahi kuweka kambi ya matibabu kisiwani Lamu wakati wa sherehe za Maulidi za kila mwaka.

Kinara huyo alisema pia huwa wanaweka kambi ya matibabu kila mwaka Al-habib Shariff Said Albeidhy anapofanya ziara mjini Mambrui.

Bw Abdushakur alisema mbali na matibabu, chama chao huwasaidia wasiojiweza kutahiri watoto wao bila malipo yoyote.

Anasema mara kwa mara, chama chao kimekuwa kikiwasaidia wasiojiweza kwa kuwashughulikia kwa matibabu ya macho na hata kwa wale wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa macho.

Kwa upande wa maradhi ya meno, mwenyekiti huyo alisema, chama hicho hutoa msaada kwa wenye matatizo ya meno, chini ya uangalizi wa Dkt George Saka.

Hivi majuzi, chama hicho kiliandaa kambi ya matibabu eneo la Shimoni, Kaunti ya Kwale na kinatarajiwa kuandaa kambi nyingine ya matibabu katika muda wa siku chache zijazo eneo la Mazeras, Kaunti ya Kilifi ambapo huduma mbalimbali za matibabu na misaada mingine itatolewa kwa wasiojiweza katika jamii.