Michezo

Supa ligi kuanza kesho Jumapili

August 31st, 2019 3 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

LIGI ya pili kwa ukubwa nchini Kenya, kwa ufupi kama NSL, itaanza kesho Jumapili kwa kukutanisha timu 20 katika viwanja mbalimbali.

Kwa jumla, msimu huu unatarajiwa kuwa mgumu zaidi baada ya timu nne kufuatana kwa karibu hadi dakika ya mwisho, msimu uliopita.

Kwa upande mwingine, vita vya kushuka daraja vitaendelea kuwa vigumu, mbali na ukweli kwamba msismko wa michuano yenyewe kuvutia.

Kutokana na utafiti wa kina, timu za Vihiga United, Nairobi City Stars, FC Talanta na Nairobi Stima ndizo zinazotazamiwa zaidi kupigania ubingwa huku nyingine zikizisindikiza.

Vihiga United ambayo ilishuka msimu uliopita, ni miongoni mwa zile zinazoitarajiwa kuzua upinzani mkali, pamoja na Nairobi Stima ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu katika NSL.

Wageni

Kulingana na ratiba, Vihiga watakuwa nyumbani ugani Mumias kupepetana na Migori Youth kuanzia saa tisa, wakati Nairobi Stima wakikabiliana na wageni katika michuano hiyo Northern Wanderers uwanjani Camp Toyoyo.

Timu kongwe Shabana FC zitaanza kutupa karata ugenini ambapo imepangiwa kucheza dhidi ya Nairobi City Stars katika uwanja wa Hope Centre, Kawangware.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, Vihiga United itaendelea kudhaminiwa na Serikali ya Kaunti ya Vihiga huku ikilenga kurejea kwa haraka kwenye ligi kuu.

Katika juhudi zake za kuikiunda upya kikosi, kocha Sammy Okoth aliwatema wachezaji 10 na kusajili 15 ambao anaamini wataisaidia timu yake kuandikisha matokeo mazuri.

Akithibitisha habari hizo, mwenyekiti wa timu hiyo, Kahi Indimuli alieleza imani yake kwa kikosi hicho ambacho pia kitapata ukufunzi kutoka kwa Nick Yakhama aliyeajiriwa kama mshauri mkuu wa idara ya kiufundi.

Vihiga ilipanda ngazi mnamo 2017, miaka mine tu baada ya kubuniwa, lakini ilikumbwa na hali ngumu katika misimu yote tangu wakati huo, kabla ya kuteremshwa.

Timu ya Mount Kenya FC ambayo pia iliteremshwa ngwazi msimu uliopita, haijajirekebisha kutokana na matatizo ya kifedha.

Msimu uliopita, timu hiyo chini ya usimamizi wa mwanasiasa Franci Mureithi ilipeana pointi za bwerere kwa klabu za Gor Mahia na Mathare United.

Awali ikiwa chini ya usimamizi wa Nakumatt Holdings, timu hii ilikuwa tisho kwa timu nyingi kabla ya kubadilisha jina.

Kwa sasa, mlezi wao, Moses Kuria ameshindwa kuirejesha baada ya kunusurika shika jingine msimu wa 2018.

Nayo Shabana kwa upande wake imejipata katika mashaka, pia kutokana na ukosefu wa kifedha na tayari wasimamizi wake wametoa mwito kwa Serikali ijitokeze kuisaidia baada ya kulemewa.

Kulingana na Katibu Mtendaji wa klabu hiyo, Stephen Kiama, Shabana inahitaji kiasi cha Sh30 milioni iliiweze kushiriki kikamilifu katika michuano yam waka huu.

Baada ya kucheza na City Stars, timu hiyo itakuwa nyumbani kucheza na Murang’a Steel ugani Gusii kabla ya kufunga safari kuelekea Mombasa kupambana na Modern Coast Rangers.

City Stars ambayo sasa iko chini ya Jackson Foundation imefanya usajili wan guvu kwa kuwaleta wachezaji kadhaa walio na uzoefu wa ligi kuu ya KPL.

Wao ni pamoja na Eric Ochieng, ambaye majuzi aliisaidia Wazito FC kupanda ngazi hadi ligi kuu ya KPL.

Mbali na kuisaidia Wazito, Ochieng aliisaidia Gor Mahia kutwaa mataji matatu ya KPL kati ya 2-13 na 2015.

City Stars ambao walimaliza katika nafasi ya 14 kadhalika wamefaulu kutwaa mlinzi matata Salim Abdalla kutoka AFC Leopards, Cornelius Mwangi, Wesley Onguso zamani mchezaji wa Gor Mahia na Sofapaka.

Wachezaji wengine wapya katika kikosi hiki ni Elvis Ojiambo, Nahashon Thiong’o ambao pia waliwahi kuchezea Gor Mahia, kipa Levis Opiyo zamani wa Mathare United na Posta Rangers.

Kadhalika klabu hiyo imewanasa Stephen Jeffa na Vincent Otieno.

Nayo, Ushuru FC itacheza chini ya kocha mpya, James Omondi aliyejaza nafasi ya Ken Kenyataa ambaye alitimuliwa baada ya msimu kumalizika. Kocha huyo wa zamani wa Muhoroni Youth analenga taji msimu huu.

Timu nyingine inayotarajiwa kuzua upinzani mkali ni FC Talanta inayonolewa na kocha mkongwe Abdalla Juma.

Ratiba ya mechi za Jumapili ni:

Ushuru na St Joseph’s Youth (Ruaraka, 3pm); Kenya Police na APS Bomet (Karuturi Sports Ground, saa saba); Modern Coast Rangers na Administration Police (Serani Sports Ground, saa tisa); Northern Wanderers na Nairobi Stima (Camp Toyoyo, saa saba); Murang’a Seal na Kibera Black Stars (Thika Stadium, saa saba); Coast Stima na Fortune Sacco (Mbaraki Sports Club, saa tisa); Nairobi City Stars na Shabana (Hope Centre, saa tisa); Bidco United na Mt Kenya United (Thika Stadium, saa tisa); FC Talanta na Vihiga Bullets (Camp Toyoyo, saa tisa); Vihiga United na Migori Youth (Mumias Complex, saa tisa).