Michezo

Super 8 yaanza wakali wakilemewa na limbukeni

March 20th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MECHI za Ligi ya Super 8 zilianza kwa kishindo wikendi iliyopita huku timu zilizowahi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo zikilemewa na timu limbukeni ambazo zilijiunga na ligi hiyo msimu huu.

Kawangware United ambao walishinda ubingwa wa 2017, waliduwazwa baada ya kupokezwa kipigo cha 5-0 na mahasimu wao kutoka eneo hilo la Dagoretti, NYSA katika mchuano uliosakatwa uwanja wa Ngong Posta.

Wenzao ambao pia wamewahi kutwaa ubingwa huo Kayole Asubuhi walishindwa kuhimili makali ya Shauri Moyo Blue Stars waliowakalifisha 1-0 mechi hiyo ikichezwa uwanja wa Calvary.

Mechi kati ya klabu ya Jericho Allstars na RYSA hata hivyo ilishuhudia mvua ya magoli Jericho wakivuna ushindi mnene wa 7-1 mechi hiyo ilisakatwa uwanja telezi ya Camp Toyoyo baada ya mvua kubwa kunyesha Jumamosi.

Mchuano huo ulishuhudia mshambulizi wa Jericho All Stars Engo Bandu akifunga mabao matatu kwa muda wa dakika nane za kwanza na kuchua uongozi wa mapema kama mfungaji bora ligini.

Wafungaji wengine kwenye kikosi hicho walikuwa ni Victor Walerah, John Awala, Warren Bosire na Caleb Olilo naye Joseph Karimi akiwafungia RYSA bao la kufutia machozi.

Katika michuano mingine limbukeni Shauri Moyo FC waliwashinda Zamalek FC ambao walimaliza nyuma ya Kawangware United mwaka 2017 3-1, Melta Kabiria wakipigwa 2-1 na Rookies Rongai All Stars uwanjani Nakeel nao Team Umeme wakiwafunga Leads United 4-0 ugani Ziwani.

Hadi sasa Jericho All Stars wanaongoza msimamo wa jedwali wakifuatwa na timu za NYSA  na Team Umeme. Zote zimesajili alama tatu japo zinatenganishwa kutokana na tofauti ya mabao.

 

Matokeo Kwa Ufupi 

Nysa 5-0 Kawangware United

Zamalek 1-3 Shauri Moyo Sportif

Jericho All Stars 7- 1 Rysa

Kayole Asubuhi 0-1 Shauri Moyo Blue Stars

Rongai All Stars 2-1 Melta

Team Umeme 4-0 Leads