Michezo

Super Eagles wa Nigeria watamla ndovu Cote d’Ivoire katika fainali?

February 11th, 2024 2 min read

JOHN ASHIHUNDU Na MASHIRIKA

KILELE cha kuwinda taji la Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023) kinafika leo Jumapili kwa pambano la fainali kati ya wenyeji Cote d’Ivoire almaarufu ‘The Elephants’ na mabingwa mara tatu Nigeria almaarufu ‘Super Eagles’ ugani Alassane Quattara mjini Abidjan kuanzia saa tano usiku.

Ni mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, huku makocha Emerse Fae wa Cote d’Ivoire na mwenzake Jose Peseiro wa Nigeria, kila mmoja akijigamba kwamba “ubingwa ni wetu”.

Kwa muda wa mwezi mmoja, mashabiki wamekuwa wakishuhudia mechi za aina yake na matokeo ya kushangaza, huku timu kubwa zikiondolewa mapema, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya mashindano haya ya mataifa Bingwa barani Afrika tangu yaanze 1957 nchini Sudan.

Ingawa Nigeria inayojivunia ulinzi imara ilifuzu kirahisi katika hatua ya mwondoano, timu hii ya kocha Peseiro haikufanya vizuri kama ilivyotarajiwa na mashabiki walioitarajia timu hiyo kupata matokeo bora zaidi.

Cote d’Ivoire ambao walifuzu kama mojawapo ya timu nne bora, walikaribia kuyaaga mashindano hayo mapema baada ya kufanya vibaya katika hatua ya makundi.

Ingawa ‘Ndovu’ wamewekewa matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa, haitakuwa rahisi mbele ya kikosi cha Super Eagles kinachojivunia mastaa kadhaa wanaosakata soka barani Ulaya.

Baada tu baada ya kutandikwa na katika mechi ya makundi, Cote d’Ivoire ilitimua kocha mkuu Jean-Louis Gasset baada wakuu wa soka nchini humo kuona kwamba hawakuwa na nafasi ya kusonga mbele

Msaidizi wake, Fae, aliteuliwa kubeba mikoba hiyo kwa muda na kushangaza wengi kufuatia ushindi wao dhidi ya Senegal na Mali katika mechi zilizofuata.

Timu hiyo ambayo ilifuzu kwa hatua ya 16-Bora kichupuchupu ilitinga fainali baada ya kuchapa DR Congo 1-0, bao lililofungwa na Sebastien Haller katika nusu-fainali ngumu iliyoshudiwa na mashabiki wengi ugani Alassane Quattara.

Sebastien Haller asherehekea kufunga bao katika nusu-fainali kati ya Cote d’Ivoire na DR Congo, uwanjani Olympique Alassane Ouattara, Abidjan, Cote d’Ivoire mnamo Februari 7, 2024. PICHA | AFP

Nigeria nao walitinga fainali baada ya kushinda Afrika Kusini kupitia kwa mikwaju 4-2 ya penalti baada ya mechi kumalizika kwa 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada, wakati wenyeji wakiilaza Mali 2-1 katika robo-fainali nyingine.

Hii ni baada ya hapo awali, kushinda Senegal 5-4 kupitia kwa hatua ya robo-fainali katika hatua ya 16-Bora, licha ya mabingwa hao watetezi kufunga la mapema mapema katika mechi hiyo iliyomaliza kwa sare ya 1-1.

Itakumbukwa kwamba Cape Verde na Equatorial Guinea zilizopuuzwa kabla ya kuanza kwa mashindano haya zilimaliza katika nafasi za kwanza kwenye makundi yao, Cape Verde iliongoza Kundi B wakati Equatorial Guinea ikimaliza kileleni mwa Kundi A.