Habari

Supkem yasubiri barua kutoka Saudi Arabia kuhusu hija

May 18th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Baraza Kuu la Waislamu ( Supkem) Hassan Ole Naado amesema kwamba bado wanasubiri barua kutoka kwa serikali ya Saudi Arabia ili kufahamu iwapo ibada ya hija mwaka 2020 itaendelea au la.

Bw Naado alieleza Taifa Leo kwamba wanasubiri mawasiliano hayo kutoka kwa Wizara ya Hija nchini Saudia na ndiyo yatatoa mwanga kuhusu suala hilo.

Kufanyika au kutofanyika kwa hija ya mwaka huu limekuwa swali vinywani mwa mahujaji kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona ambavyo vimelemeza shughuli nyingi katika mataifa kadhaa duniani.

Saudia ni kati ya mataifa yaliyoathirika na virusi hivyo huku watu 312 wakiripotiwa kufariki na wengine zaidi ya 55,000 wakiambukizwa corona.

Mnamo Februari serikali ya Saudia ilipiga marufuku ibada kwenye maeneo matakatifu kwenye miji ya Mekka na Madina kama njia kuzuia kuenea kwa virusi hivyo hatari.

Ikizingatiwa kwamba mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kukamilika Jumapili hii au Jumatatu ijayo kulingana na mwandamo wa mwezi, itakuwa imesalia miezi miwili pekee kabla ya kuandaliwa kwa hija.

“Kama Supkem tulimaliza kazi yetu kwa kupiga msasa na kuidhinisha orodha halali ya maajenti ya kuwahudumia mahujaji. Tutajua kama ibada ya Hija mwaka 2020 itafanyika au kukosekana baada ya kupokea barua kutoka kwa Wizara ya Hija. Tunaisubiri taarifa hiyo. Iwapo hija itafanyika basi naamini mahujaji wetu wamejitayarisha mapema. Hatufai kuharakisha mambo dakika za mwisho mwisho,” akasema

“Virusi vya corona vimevuruga matukio mengi na hata kusababisha kusitishwa kwa safari katika maeneo takatifu ndiyo maana mawasiliano hayo ndiyo yatatoa mwelekeo kuhusu hija,” akaongeza Bw Naado.

Mchakato wa kuhudhuria ibada hiyo huhusisha mahujaji kutafuta pasipoti za usafiri na kulipa fedha zinazohitaji kugharimia safari za ndege, malazi na vyakula kupitia maajenti wao.

Ibada ya hija huchukua siku tatu na kilele chake huwa sikukuu ya kuchinja ya Eid al-Adha.

Mwaka 2019 zaidi ya Wakenya 4,500 walihudhuria ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya dini ya Kiislamu.