Habari Mseto

Sura ya Mzee Kenyatta yazua utata wa noti mpya

June 3rd, 2019 1 min read

CECIL ODONGO na RICHARD MUNGUTI

UTUMIZI wa noti mpya zilizozinduliwa Jumamosi na Benki Kuu ya Kenya (CBK) umeendelea kupingwa na viongozi pamoja na baadhi ya wananchi, ambao hawafurahishwi na picha ya sanamu ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta.

Jana, Mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Bw Simon Mbugua na mwanaharakati Okiya Omtatah waliwasilisha kesi kortini kupinga utumizi wa noti hizo.

Hatua yao ilitokea siku moja tu baada ya viongozi wakuu wa Chama cha ODM kueleza jinsi kuwepo kwa sura ya Mzee Kenyatta kwenye noti hizo ni ukiukaji wa katiba ambayo ilipiga marufuku sura ya mtu yeyote kutumika kwenye sarafu za Kenya.

Wikendi, Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw James Orengo alieleza kujitolea kwake kushiriki kwenye kesi itakayopinga noti hizo kortini.

Katika kesi waliyowasilisha katika Mahakama kuu ya Milimani, Nairobi, Bw Mbugua na Bw Omtatah pia walisema hatua ya Gavana wa CBK, Dkt Patrick Njoroge kutangaza kuharamishwa kwa noti za sasa za Sh1,000 ifikapo Oktoba 1, 2019 ni kinyume na katiba.

“Hatua ya CBK kuchapisha noti mpya ya Sh1,000 ikiwa na picha ya mwanzilishi wa taifa hili Mzee Jomo Kenyatta inakinzana na katiba inayosema sarafu za Kenya ziwe na alama ya turathi ambayo inaonyesha umoja na mshikamano wa jamii,” amesema Bw Mbugua.

Hata hivyo, Dkt Njoroge jana alisema yupo tayari kukabiliana mahakamani na wanaopinga matumizi ya noti hizo.

Kulingana naye, utaratibu wa kikatiba ulifuatwa na vilevile umma ukashirikishwa kabla ya kuamua jinsi noti mpya zingekuwa.

Dkt Njoroge alitangaza kuwa Wakenya wanaopanga kubadilisha kati ya Sh1 milioni hadi Sh5 milioni na wana akaunti za benki watalazimika kufika kwenye matawi ya benki zao kuzibadilisha bila masharti yoyote.

Wale wenye nia ya kubadilisha Sh5 milioni na zaidi watalazimika kupata kibali kutoka kwa CBK lakini watachunguzwa kwa kina kuhusu utajiri wao.