Sutton athubutu kusema Salah anapiku Ronaldo na Messi katika orodha ya wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa

Sutton athubutu kusema Salah anapiku Ronaldo na Messi katika orodha ya wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa

Na MASHIRIKA

FOWADI wa zamani wa Blackburn Rovers, Chris Sutton, amekiri kwamba Mohamed Salah ndiye mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa na kuibua mjadala kuhusu iwapo kweli sogora huyo wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri anawapiku Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Kwa mujibu wa Alan Shearer ambaye ni mfumaji wa zamani wa Uingereza, bao la Salah dhidi ya Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 3, 2021 ni mojawapo ya magoli bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika ulingo wa soka enzi hii.

Hadi kufikia sasa, Salah, 29, amefungia Liverpool mabao tisa kutokana na mechi tisa msimu huu.

“Katika kipindi hiki cha sasa, Salah ndiye mchezaji bora zaidi duniani. Mgongo wake unasomwa na Ronaldo kisha Messi,” akasema Sutton kwa kusisitiza kwamba itawachukua Kylian Mbappe na Neymar muda mrefu zaidi kabla ya kuanza kulinganishwa na watatu hao.

Baada ya kufunga bao lake la 100 katika EPL mnamo Septemba, Salah alifunga mojawapo ya magoli yake bora zaidi dhidi ya Manchester City katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na Liverpool dhidi ya mabingwa hao watetezi mnamo Oktoba 3, 2021 ugani Anfield.

“Kinachomweka Salah mbele ya Ronaldo na Messi ni uthabiti wake wa kipindi kirefu. Mchezo wake unatabariki na makali yake hayashuki ovyo. Ni mchezaji wa kutegemewa uwanjani na fursa nyingi anazozipata huishia kuzaa mabao,” akaeleza Sutton.

Mbali na kufunga mabao tisa hadi sasa, Salah ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea na AS Roma, pia amechangia mabao matatu kambini mwa Liverpool muhula huu.

Anajivunia wastani wa mabao 21 kila msimu katika kipindi cha mihula mitatu iliyopita katika kampeni za EPL na msimu wa 2017-18 ndio uliomshuhudia akifunga magoli mengi zaidi ligini (32).

“Si rahisi kwa mwanasoka yeyote kuendeleza uthabiti huo katika soka ya sasa ambayo ina ushindani mkali,” akaongeza Sutton katika kauli iliyoungwa mkono na beki Micah Richards aliyewahi kuchezea pamoja na Salah kambini mwa Fiorentina ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2015.

Kufikia sasa muhula huu, Neymar amefungia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) bao moja pekee kutokana na mechi tisa za kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Kwa upande wake, Messi amefungia miamba hao wa Ufaransa goli moja pekee la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Man-City.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Familia ya Glazer kuuza hisa 9.5 milioni za Man-United kwa...

KAMAU: Tamaa imegeuza Afrika kuwa ‘soko la utumwa’