Makala

SWAGG: Cardi B

April 9th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

BELCALIS Almanzar likiwa ndilo jina alilopewa Cardi B alipozaliwa, sio demu wa levo ya kila mtu.

Ana urembo wa kupagawisha, ana shepu ya kutamanisha, ni rapa hatari, ana pesa za kumwaga na hata zaidi ni maarufu.

Kwa kifupi humwambii kitu kama hauna vigezo hivyo.

Umaarufu wake Cardi kaupata kupitia muziki lakini hadi anafikia upeo alio nao kwa sasa, kimekuwa ni kibarua kigumu.

Cardi B aipokea tuzo Februari 10, 2019, kwenye makala ya 61 ya Tuzo za Grammy mjini Los Angeles. Picha/ AFP

Alipata umaarufu mkubwa kwenye gemu ya rapu alipoachia hiti yake ya ‘Bodak Yellow’ na ndiyo kazi iliyomfungulia milango ya rehema na kumpa heshima yake kwenye Hip Hop.

Kupitia uwezo aliouonyesha kwenye kazi hiyo, ameweza kupata fursa kibao kushirikiana na mastaa wengine wakubwa kama Nicki Minaj, Migos kati ya wengi wengineo katika kufanya kolabo.

Toka kazi hiyo ya Bodak Yellow’ ivume Cardi B ameweza kuachia kazi zingine kadhaa kama ‘Sauce Boyz’, ‘Foreva’, ‘Motorsport‘, ‘Bartier Cardi’ hivyo kumwezesha kukamata nafasi yake kwenye chati za Hip Hop Marekani.

Pochi

Kutokana na mafanikio ya Bodak Yellow’ utajiri wa Cardi B ulipanda maradufu kutoka dola 600,000 (Sh60 milioni) hadi dola 4 milioni (Sh402 milioni).

Lakini ukiachia mbali muziki pia Cardi B kaingiza pesa kwa kuigiza kwenye kipindi maarufu kule Marekani Reality Show ya Love & Hip Hop Atlanta.

Huu ni mwanzo tu wa safairi yake ya kujigeuza tajiri kama marapa wengine na kuna uwezekano takwimu hizo zitapanda hata zaidi ndani ya miaka michache ijayo.

Usafiri

Cardi B mara si moja katoa kauli za kujigamba jinsi alivyo mrembo na tajiri. Na kwa yeyote anayeweza kutaka kukadira utajiri wake basi atalazimika kuanza kwa kukadiria thamani ya magari anayoendesha kama lile aina ya Rolls Royce lenye thamani ya dola 400,000 (Sh40 milioni), na pia Bentley iliyomkosti dola 240,000 (Sh24 milioni)

Mjengo

Ukiwa tu katika masuala ya hela, mtoto wa kike vile vile anamiliki mjengo wa uhakika kule New Jersey unaoweza kufananishwa na hoteli ya 5 Star.


Alikuwa stripa

Hii ni kazi aliyoifanya toka alipokuwa tineja kabla ya umaarufu. Cardi B alianza kusaka maisha akiwa tineja mwenye umri wa miaka 18 na kazi yake ya kwanza kufanya ilikuwa ni ustripa mle vilabuni. Taarifa zinadai kwamba Cardi B alipanga kustaafu kazi ya ustripa ambayo huhusisha zaidi kutoa burudani kwa wateja kwa kudensi ukiwa uchi au nusu uchi, wakati angehitimu umri wake wa sasa wa miaka 25. Hata hivyo, aliishia kuikacha akiwa na umri wa miaka 23 baada ya kujiunga na Reality Show ya Love & Hip Hop Atlanta.

Usilolijua

Jina lake la stejini Cardi B alipachikwa na wazazi wake. Babake anatokea taifa la Dominic Republic huku mamake akitokea visiwa vya Trinidad & Tobago lakini wamemlelea kule mjini New York. Wazazi wake ndio waliompa jina lake la stejini kwa kumwita Bacardi ili kudumisha asili yake ya watu kutoka jamii ya Caribbean. Baadaye Bacardi aliamua kubadilisha na kujiita Cardi B.

Uhusiano wa kimapenzi

Yupo kwenye mahusiano na rapa Offset anayetokea kundi la Migos ambaye alimchumbia 2017 kwa kumvisha pete yenye thamani ya dola 500,000 (Sh50 milioni) na kisha baadaye wakaoana.

Waliishia kutengana miezi michache baadaye baada ya kuibuka kuwa Offset alimchepukia, ikiwa ni baada ya kuvuja kwa mkanda wa ngono ukimwonyesha akiwa na mwanamke tofauti na Cardi B.

Baada ya kutemana, Cardi B alisema hataitisha talaka. Mwaka 2019 wametangaza kurejesha tena penzi lao na kwa sasa wanaishi kama mke na mume kama hapo awali huku wakimlea binti yao mmoja.

Swagg

Kutokana na kazi yake ya awali ya ustripa, unaweza ukaelewa mtindo wa fasheni wake Cardi B. Huacha sehemu zake za mwili zikiwa wazi. Anapenda kuvalia mavazi ya ‘kichokozi’ muda mwingi.