Makala

SWAGG: Chris Evans

July 2nd, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

CHRISTOPHER Robert Evans al-maarufu Chris Evans ni miongoni mwa waigizaji maarufu wanaojulikana kwa uhusika wao kwenye filamu za ‘superhero’.

Kwa shabiki makini wa filamu za sampuli hii, Chris hatakuwa mgeni sana kwake na hata pengine huenda akawa ndiye mwigizaji wake bora.

Sanaa

Chris ambaye katisha sana kwenye filamu kibao za ‘superhero’ zilizotayarishwa na kampuni ya Marvel, alianza taaluma yake ya uigizaji miaka 19 iliyopita akitokea kwenye kipindi cha televisheni Opposite Sex kilichopata umaarufu mkubwa kule kwao Marekani.

Hii ilikuwa ni baada yake kufuzu katika masomo ya uigizaji kutoka Taasisi ya uigizaji Lee Strasberg iliyoko mjini New York.

Baada ya kufuzu alianza kusaka kazi na akabahatika kuangukia uhusika mdogo wa filamu kadhaa zilizomsaidia kukomaa taratibu.

Taratibu aliendelea kupata mchongo wa kuigiza kwenye filamu mbalimbali zikiwemo komedi.

Hata hivyo jina lake kwenye gemu lilianza kupata uzito alipopata mchongo wa kutokea kwenye filamu ya Fantanstic Four (2005).

Aliendelea na pilkapilka zake hadi akaishia kuangukia dili ya kuwa mmoja wa wahusika kwenye misururu ya filamu za Avengers. Uhusika wake kwenye filamu hizi ulitokana na filamu aliyoigiza kama staa ya Captain America.

Na huku msururu wa Avengers ukiwa umemalizika mwaka 2019 kwa ile ya Avengers: End Game, Chris tayari keshajipanga.

Novemba 2019 ataingiza sokoni filamu yake mpya The Red Sea Diving Resort akivalia uhusika wa jasusi hatari kutoka kitengo cha upelelezi cha Israeli kifahamikacho kamo Mossad.

Pia ana kazi nyingine Knives Out iliyoratibiwa kuachiwa baadaye mwaka 2019.

Mkwanja

Kwa uhusika wake kwenye filamu hizi za Marvel, Chris kukafunga kinoma. Utajiri wake umekadiriwa kufikia dola 50 milioni.

Mwaka 2018 alitengeneza dola 34 milioni kama mshahara kabla ya makato ya kodi.

Alipotokea kwenye Avengers: Age of Ultron (2015), alilipwa dola 13.5 milioni. Ilipotoka Avengers: Infinity War (2017), alilipwa dola 18 milioni.

Maskani

Anamiliki mjengo wa nguvu kule Atlanta mji anaosemekana kuupenda kweli kweli na ndio sababu yake ya kuwa na maskani kule.

Mjengo huo aliununua kwa thamani ya dola 3.5 milioni. Kwa namna ilivyoundwa, utadhani ni mojawapo wa hoteli za kitalii zenye haiba yake. Mjengo huo upo mlimani na ndani kuna bustani ya kupendeza ya miti na maua kibao. Pia una kidimbwi cha kuogelea huku baadhi ya kuta zake zikiwa za vioo kwa ajili ya kumpa uwezo wa kufurahia mandhari aliyojitengenezea.

Usafiri

Kwa usafiri wake wa mijini, jamaa anamiliki mikebe ya bei mbaya ukianza na Ferrari, Lexus, Benz, Chevrolet Camaro (1967) na Range Rover.

Uhusiano

Chris ni sukari ya warembo unaambiwa ila mwaka 2019 toka ulipoanza hajaweza kuonekana akiwa na demu yeyote.

Hata hivyo, wapo wanaoamini kuwa ana mtu sema ameamua kumweka siri sana.

Mwanamke wa mwisho kuhusishwa naye alikuwa mwigizaji mwenza Jenny Slate aliyeonekana sana naye mwaka 2018 ila wakaishia kuachana.

Wanawake wengine aliotoka nao ni Elizabeth Oslen ambaye pia ni mwigizaji, kichuna Lily Collins aliyekuwa na uhusiano naye mwaka 2015, Lucy Pinder ambaye ni mwanamitindo wa Uingereza pia alitoka naye 2015.

Chris pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na staa mwigizaji Sandra Bullock 2014 kabla ya msupa huyo kuolewa 2015 na mumewe Bryan Randall.

Aliwahi pia kutoka na kichuna Sacha Kemp 2011. Mwaka wa 2008, aliingia kwenye mahusiano na vichuna wawili Vida Guerra na baada ya kutemana naye akamdandia Kristin Cavallari.

Kabla ya kuvuka na hao, 2007 alikuwa kwenye uhusiano na Christina Ricci.

Mrembo Minka Kelly ndiye aliyedumisha uhusiano naye kwa muda mrefu sana toka 2007 hadi 2014 wakiwa na mazoea ya kutemana na kurudiana. Kabla ya kuanzisha mahusiano na Kelly, alikuwa na uhusiano mwingine na Gisele Bundchen 2006.