Makala

SWAGG: Emily Bett

May 7th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

EMILY Bett Rickards ni kati ya waigizaji wachanga wanaokuja kwa kasi ya Usain Bolt.

Akiwa na umri wa miaka 27 pekee, mwigizaji huyu ameweza kujiweka kwenye ramani ya waigizaji wengine wa kike wanaoheshimika kwa kazi zao.

Emily ni mwigizaji stadi, anapenda kuvalia uhusika wenye ucheshi na hata zaidi ni mrembo wa kufa mtu.

Ni kichuna anayependa anachokifanya na katika kulifanya, ameweza kujitengenezea mkwanja wa maana.

Pochi

Kwa mwigizaji wa rika lake kuweza kujikusanyia utajiri unaokadiriwa kuwa unafikia thamani ya dola 4 milioni (Sh400 milioni), hiyo ni hatua nzuri ya mafanikio. Makadirio hayo yalifanywa na Celebrity Net Worth 2019.

Mkwanja wake umetokana na uigizaji wake huku kiasi kikubwa kikichangiwa na uhusika wake wenye Series ya ‘Arrow’ ambayo imechangia pakubwa kumpa umaarufu.

Kwa kipindi cha miaka saba ambacho amekuwa na ‘Arrow” Season 1-7, kila mwaka Emily ambaye kavalia uhusika wa Felicty Smoak au Overwatch, alilipwa kati ya dola 800,000 na dola 900,000 (Sh80-90 milioni).

Mbali na uigizaji, pia ameweza kupiga fedha za ziada kwa kuwa balozi wa jarida la Bello Magazine.

Historia ya Sanaa

Emily alizaliwa nchini Canada ingawaje asili yake kamili ni Colombia.

Babake ni daktari jijini Vancouver; jiji kuu la Canada.

Baada ya kufuzu kidato, alijiunga na Chuo cha Uigizaji cha Vancouver Film School. Aliishia kutokea kwenye kazi yake ya kwanza 2009, alipohusika kwenye video ya muziki ya Nickleback, bendi ya Rock kutoka Canada.

Emily alishiriki sana kwenye vipindi vya televisheni akitokea kama muhusika mdogo. Milango yake ya nuru ilifunguka 2012 alipopata fursa ya kuigiza kwenye ‘Arrow’ alikovalia uhusika wa mtaalamu wa kompyuta.

Mwanzoni, uhusika wake ulipangiwa kuwa wa episodi moja, ila kutokana na kiwango alichokionyesha hasa ucheshi na mwingiliano mzuri na Stephen Amell anayevalia uhusika wa Oliver Queen, maprodusa wakaamua kumwongezea kazi zaidi kufuatia mapokezi makubwa ya mashabiki.

Hivyo ndivyo nyota yake ilivyozidi kung’aa.

Kuwa kwenye kazi hiyo kulimfungulia michongo zaidi akitokea kwenye filamu zingine kadhaa kama vile ‘Romeo Killer: The Chris Porco Story’, Series ya ‘Flash’, kati ya zingine kibao.

Michongo hiyo ndiyo imeweza kumweka kwenye ramani ya kukubalika na mastaa mbalimbali.

Mijengo

Kutokana na mafanikio yake pamoja na kwamba mara nyingi anajikuta akisafiri hadi Marekani kikazi, Emily kalazimika kununua jumba la kifahari ugeninini.

Anamiliki jumba la kifahari maeneo ya Los Angeles, Califorinia. Pia ana jumba lingine la bei mbaya mjini Vancoveur.

Usafiri

Kama tu mastaa wenzake, Emily huzunguka kitaa na mikebe ya nguvu kama vile Ferrari na Audi.

Mahusiano

Emily amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa miaka kadhaa sasa na staa mwenzake Colton Hayes.

Hayes ameigiza kwenye filamu kadhaa kubwa kubwa kama vile ‘Vampires Diary’, ‘Teen Wolf’ na pia yupo kwenye ‘Arrow’.

Wawili hao walikutana Disemba 2013 kwenye series hiyo na kuanzisha uhusiano uliodumu mpaka sasa licha ya kuwa waliripotiwa kutengana baada ya mwaka mmoja pamoja.

Kwenye posti kadhaa za Hayes, ameishi kummiminia sifa kibao kichuna huyo kiasi cha kusema kuwa daima atabakia kuwa mke wake hata ikiwa ataishia kutoka na mwanamume mwingine.