Makala

SWAGG: Jason Momoa

May 28th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

MIONGONI mwa waigizaji mastaa wa kiume wenye mvuto wanaomezewa mate na vidosho kibao ulimwenguni ni Joseph Jason Namakaeha Momoa.

Jason kaanza kupata umaarufu yapata miaka mitano au sita hivi iliyopita baada ya jitihada zake za miaka mingi kulipa.

Utangulizi

Jason alizaliwa miaka 40 iliyopita kule Honolulu, Hawaii mojawapo ya majimbo ya Amerika.

Unaweza kusema kuwa wazazi wake walikuwa wasanii, mamake akiwa ni mpiga picha naye babake akiwa mchoraji wa kutumia rangi. Wazazi wake hawakujaliwa kupata mtoto mwingine zaidi yake.

Akiwa chuoni, alisomea baolojia inayohusiana na mazingira ya majini.

Katika maisha yake, amebahatika kusafiri sana kote duniani na kwenye safari hizo aliishia kutambulishwa kwenye dini ya ‘Buddhism’ nchini Tibet.

Ni dini anayoifuatiliwa kwa ukaribu sana mpaka wa leo.

Taaluma

Kipaji chake cha kuigiza kilitambuliwa na mwanamitindo Takeo Kobayashi mwaka 1998.

Kobayashi alimshawishi sana ajaribu kuwa mwanamitindo.

Mwaka mmoja baadaye akajiunga na tasnia hiyo na kuishia kutwaa taji la Hawaii Model of the Year 1999.

Mwaka uliofuatia aliangukia dili ya kuigiza kwenye kipindi cha televisheni Baywatch Hawaii.

Kufikia 2003, alikitosa kipindi hicho na kuibukia kwenye kingine Johnson Familly Vacation.

Hata hivyo, milango ya nuru katika tasnia ilimfungukia vyema alipopata mchongo na kuvalia uhusika wa Khal Drogo kwenye msururu wa kipindi maarufu cha Game of Thrones, 2011.

Baadaye alipata mchongo wa kuigiza kwenye filamu ya Batman Vs Superman: Dawn of Justice (2016) na Aquaman (2018) nazo zikamtangaza hata zaidi.

Aidha 2017 alihusika kwenye filamu za Justice League na Once Upon a Time in Venice.

Mkwanja

Kipato chake kwa ujumla kinakadiriwa kuwa kati ya dola 8-14 milioni kwa mujibu wa majarida mbalimbali.

Mkwanja wake wote umetokana na malipo anayoingiza kupitia uigizaji.

Mjengo

Anaishi kwenye jumba la kifahari kule Los Angeles pamoja na familia yake.

Mjengo huo uliojengwa kwenye ploti ya ekari tano unamilikiwa na mke wake, Lisa Bonet.

Lisa alihamia kwenye mjengo huo na bintiye Zoe akiwa na umri wa miaka mitano baada ya ndoa yake kwa mwanamuziki Lenny Kravitz kuvunjika.

Usafiri

Anapenda mashine za maana na ndio sababu yake ya kumiliki mikebe kadhaa yenye adabu. Anayo Land Cruiser 1978, Range Rover, Mercedes Benz kati ya nyinginezo.

Mahusiano

Kwenye Baywatch (1999), Jason alikutana na mwigizaji Simmone Mackinnon na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi naye. Mwaka 2004 alitangaza kumchumbia na miaka miwili baadaye uhusiano wao ukavunjika.

Mwaka 2005 ukiwa mwaka mmoja kabla ya kutemana na Simmone, alikutana na mwigizaji mwingine – Lisa Bonet – kwenye shughuli za kikazi. Walibakia washikaji ila baada yake kutemana na Simmone, alianzisha uhusiano na Lisa anayemzidi umri kwa miaka 12.

Wawili hao walifunga ndoa 2017 wakiwa tayari wamejaliwa watoto wawili.

Hata hivyo Momoa pia ni baba wa kambo wa binti Zoe, aliyezaliwa kutokana na ndoa ya awali ya mamake iliyovunjika.