Makala

SWAGG: Juicy J

June 11th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

JORDAN Michael Houston al-maarufu Juicy J ni rapa, mtunzi mashairi na produsa wa muziki kule Amerika.

Ni mwanachama wa kundi la Hip hop Three 6 Mafia. Kando na kuwa kundini, yeye binafsi ameachia albamu zake kadhaa.

Kakake mkubwa Project Pat naye vilevile ni rapa.

Juicy J amekuwa kwenye muziki kwa miaka mingi na kando na kutunga muziki wake, ameweza pia kuprodusi kazi kibao za wasanii wakubwa.

Maisha

Juicy alizaliwa Aprili 1975 ikiwa ni miaka 44 iliyopita kule Memphis, Amerika. Baba yake alikuwa ni mhubiri.

Mapenzi yake ya muziki yalianza akiwa tineja. Alipenda sana kusoma vitabu na majarida ya burudani ili kujiweka sawa na ufahamu wa jinsi showbiz ilivyokuwa ikiendelea. Ni kwenye harakati hizo ambapo pia mapenzi yake ya kucheza ala mbalimbali za muziki yaliibukia.

Aanza sanaa

Baada ya kukamilisha elimu ya sekondari mwaka 1991 alianzisha kundi la Hip hop Three 6 Mafia kwa kuwaleta pamoja wasanii watano.

Miaka michache baadaye, yeye pamoja na mmoja wa wanachama kundi DJ Paul walianzisha kampuni yao ya burudani Prophet Entertainment. 1994 walimwachia lebo hiyo Nick Scarfo na kuanzisha kampuni nyingine Hypotize Minds.

Wakiwa kama kundi, Three 6 Mafia waliachia albamu yao ya kwanza Mystic Stylez (1995) na huo ukawa mwanzo wao. Toka kipindi hicho kundi hilo limeachia albamu nane. Mnamo 2002 alidondosha albamu yake ya kwanza akiwa msanii solo Chronicles of the Juice Man.

Miaka saba baadaye toka alipoachia albamu hiyo, alijitenga na kundi lake la Hip hop ili kutilia mkazo taaluma yake ya muziki kama msanii solo mpaka leo hii.

Mkwanja

Utajiri wake unakadiriwa kuwa wa dola 30 milioni. Sehemu kubwa ya mkwanja wake ikitokana na kundi la Three 6 Mafia lililokuwa maarufu kumliko kabla hajajitoa na kuja kuvuma kama msanii solo.

Lakini kipato hicho kimechangiwa na mishahara ya kuwaprodusia muziki wasanii mbalimbali wakiwemo mastaa kama vile Wiz Khalifa, Nicki Minaj, Ludacris, na kakake Project Pat.

Mjasiriamali

Juicy J pia kaingiza kipato kupitia uwekezaji kwenye biashara mbalimbali. Kando na mapato anayopiga kupitia kampuni yake ya Hypnotize Minds kwa ushirikiano na DJ Paul, pia anaingiza mkwanja kutoka kwa lebo ya Wiz Khalifa Taylor Gang Entertainment ambapo pale yeye ni mwanahisa.

Miaka minne iliyopita, alifanya uwekezaji mwingine kwa kununua hisa kwenye kampuni ya maji, Core Hydration Premium. Kwa sasa thamani ya kampuni hiyo inatajwa kuwa dola 525 milioni.

Jumba

Kwa miaka mingi aliiishi kwenye nyumba ya kifahari jiji la Memphis alikozaliwa. Aliamua kuuza mjengo huo 2012 kwa dola 580,000.

Baada ya hapo alihamia California na kununua mjengo mwingine wa nguvu katika maeneo ya kifahari ya Beverly Hill wanakoishi mastaa kibao wa sanaa.

Usafiri

Kati ya mikebe yake ya nguvu anayomiliki ipo Rolls Royce Phantom aliyoinunua kwa dola 145,000 (Sh14.5 milioni) na Bentley Mulsanne yenye thamani ya dola 300,000 (Sh30 milioni).

Mahusiano

Tofauti na wasanii wengine maarufu wanavyopenda michepuko, Juicy J amesalia na demu mmoja kwa miaka mingi hata kabla ya kuwa maarufu.

Alichumbiana na kisura wake huyo Regina Perera Julai 2016. Walifuatisha na harusi ya kimya kimya na mwaka mmoja baadaye wakafanikiwa kupata mtoto.

Juicy huwa msiri sana na maisha yake ya kibinafsi.

Usilolijua

Kwenye ulingo wa Hip hop anaweza akawa sio maarufu sana kuwaliko mastaa watajika wanaofahamika ila ndiye rapa wa kwanza kutwaa tuzo ya Oscar kwenye kitengo cha Hip-hop Act.