Makala

SWAGG: Master P

June 18th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

KWA kizazi cha sasa, ni wachache watakuwa wanamfahamu rapa Percey Robert Miller al-maarufu Master P.

Ila kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa Hip Hop, Master P ni miongoni mwa marapa maarufu duniani na ni tajiri kwelikweli.

Umaarufu wake umetokana na muziki, uliochangia utajiri wake. Lakini hatua ya kujitosa kwenye sanaa ya uigizaji na ujasiriamali, imemzidishia utajiri si mchezo.

Anaweza akawa hayupo kwenye levo ya Jay Z, ila hamna kitu cha kawaida kinachonunuliwa kwa mkwanja mrefu kinamshinda Master P.

Kwa kifupi, naye kakafunga kukafunga unaambiwa.

Maisha

Master P alizaliwa Aprili 1970 kule New Orleans, Louisiana miaka 49 iliyopita.

Rapa huyu alizaliwa kwenye mtaa uliosifika kwa uhalifu zaidi ya kitu kingine.

Wazazi wake walitalikiana akiwa bado mdogo na kujikuta akilelewa na babake mzazi pamoja na ndugu zake wanne.

Kulingana naye, kupata msosi ilikuwa noma pale nyumbani hivyo alijikuta akipitia maisha magumu kweli kweli.

Ndoto ya ujasiriamali

Akiwa kwenye mahangaiko hayo, wazo la kuwa mwanabiashara lilimshika mguu akiwa bado mdogo.

Hii ilikuwa ni baada ya jirani mmoja wao aliyekuwa akifanya kazi ya afisa mauzo, kurejea mtaani akiwa na Mercedes Benz mpya.

Kwa kuwa alikuwa anamfahamu sana, kitu hicho kilimkuna kichwa Master P na hapo akaanza kuwazia ujasiriamali akiamini ndo ungemfungulia njia na kumkwamua kutoka umaskini.

Akiwa kidato akaanza biashara ndogo ya kuuza simu.

Master P anasema hakuna ndugu yake yeyote aliyefanikiwa kupata ajira na ndio sababu akaamua kujaribu kujiajiri.

Aanzisha lebo yake

Katika miaka ya tisini (1990s), alianzisha lebo yake No Limit Records akiwa kama produsa na msanii. Mtaji wa kuanzisha alitoa kutoka kwenye urithi wa bima wa babu yake aliyemwachia dola 10,000 (Sh1 milioni).

Kisha alifungua duka la kuuza muziki wake pamoja na wasanii wengine.

Tayari alikuwa ameshaanza kuachia nyimbo zilizoishia kumpa umaarufu mkubwa miaka hiyo.

Baada ya kuona muziki wake umekaa sawa, akaamua kuutumia kujiendeleza kibiashara zaidi.

Biashara kibao zafuata

Hapo kwa kutumia mtaji aliokuwa amekusanya kupitia muziki, akaanza kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.

Anamiliki kampuni ya usimamizi wa michezo, anayo ya mavazi ya brandi yake, huduma za usafiri, ya uuzaji simu aliyoanzisha zamani, ya Video Games na pia anayo Studio ya utengenezaji wa Filamu.

Vile vile alipanua biashara ya lebo yake ya muziki ambayo ameibadilisha jina mara kadhaa kwa sasa ikifahamika kama No Limit Forever Records. Kwa sasa lebo hiyo inasimamiwa na vijana wake wawili Valentino na Romeo huku yeye akishughulika na biashara zinginezo.

Master P ana jumla ya kampuni 45.

Utajiri

Kufikia mwaka huu 2019, utajiri wake umekadiriwa kuwa dola 250 milioni.

Kupitia lebo yake ya muziki, ameweza kuingiza jumla ya dola 160 milioni huku salio kwenye hesabu hizo zikijalizwa na biashara zingine.

Majumba

Unaambiwa anamiliki jumla ya majumba 31 ya kifahari mengi yakiwa ya kupangisha. Baada ya kutalikiana na mke wake 2014, mama huyo Sonya Miller aliitaka Mahakama impe majengo manane kati ya hayo 31.

Usafiri

Hapa ndio usiseme. Anamiliki zaidi ya magari 13 ya bei mbaya yakiwemo Roll Royce, Porsche, Jaguar, Escalade, Bentley miongoni mwa mengine.

Rolls Royce. Picha/ Hisani

Tuzo

Kashinda tuzo za Grammy Awards mara tano, moja ya BET na nyingine ya VH1.