Swara tena EPL

Swara tena EPL

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

WASIMAMIZI wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamejipiga moyo konde na kusisitiza hawana mipango ya kusimamisha msimu wa 2020-2021, licha ya ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Mnamo Jumatatu, mchuano wa ligi kati ya Manchester City na Everton uliahirishwa saa nne kabla ya kung’oa nanga kwa sababu ya mkurupuko wa corona.

City ilisitisha shughuli zake zote siku hiyo baada ya visa kadhaa vya virusi hivyo kutokea kambini mwake.

Hata hivyo, kwa sasa wachezaji wamerejea mazoezini baada ya kukosekana kwa kisa cha maambukizi katika vipimo vilivyofanywa Jumanne.

Mnamo Jumanne, watu 18 katika ligi hiyo ya klabu 20 walipatikana na corona baada ya vipimo vya hivi punde.

Visa vipya kambini mwa timu ya Fulham vilisababisha mechi dhidi ya Tottenham Hotspur, iliyoratibiwa kusakatwa Jumatano, kufutiliwa mbali.

Sheffield United pia ilithibitisha kuwa “ilikuwa na visa vingi vya corona kambini mwake” katika vipimo hivyo vya hivi punde.

Kocha wa West Brom, Sam Allardyce, ametaka soka isitishwe kwa muda lakini wasimamizi wa ligi walisisitiza kuwa EPL “haijajadiliana kuchukua uamuzi kama huo”.

“Ligi ina imani katika masharti yake ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi hivyoi vya corona, kuhakikisha mechi zinaendelea jinsi zilivyopangwa, na masharti haya yanaungwa kwa dhati na serikali,” ilisema EPL.

“Huku tukiweka kipaumbele afya ya wachezaji na maafisa wa mechi, ligi pia inaunga mkono kikamilifu jinsi klabu zinatekeleza maagizo yaliyowekwa kudhibiti uenezaji wa virusi vya corona.”

Ingawa ligi inafaa kuendelea jinsi ilivyopangwa, mashabiki hawataruhusiwa tena kuhudhuria mechi huku maeneo mengi nchini Uingereza yakiwekewa masharti makali usiku wa kuamkia jana.

Mji wa Liverpool umetiwa katika orodha ya tatu ya maeneo yanayotakiwa kufuata masharti makali; kumaanisha kuwa mashabiki hawataruhusiwa uwanjani Anfield kushabikia timu ya Liverpool, wala ugani Goodison Park kuona kikosi cha Everton kikicheza.

Viwanja hivyo ndivyo pekee vya Ligi Kuu mjini Liverpool ambavyo vilikuwa vimekubaliwa kuwa na mashabiki 2,000 ila kwa masharti mepesi ya orodha ya pili.

Maeneo mengi Uingereza yamewekwa chini ya masharti makali ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, baada ya visa 50,023 na vifo 981 kuripotiwa nchini humo Jumatano.

Isitoshe, aina mpya ya kirusi cha corona ambayo imechipuza hivi majuzi pia imeripotiwa kuingia na kuanza kusambaa Uingereza.

Leo itakuwa zamu ya Everton na Manchester United kualika West Ham na Aston Villa mtawalia, kwenye ligi.

Everton haijapoteza dhidi ya West Ham katika mechi nne zilizopita – imeshinda mara tatu na kutoka sare moja.

Hivyo, itajibwaga nyumbani Goodison Park ikipigiwa upatu kuandikisha matokeo mazuri. Vijana wa Carlo Ancelotti watakuwa wakifukuzia ushindi wa tano mfululizo ligini msimu huu; hii ni baada ya kulemea Chelsea, Leicester, Arsenal na Sheffield United katika mechi zilizopita.

West Ham haina ushindi katika michuano minne iliyopita baada ya kupiga sare dhidi ya Crystal Palace, Brighton na Southampton huku ikipoteza mikononi mwa Chelsea.

Mashetani wekundu wa Manchester United wanatarajiwa kupimwa vilivyo makali yao watakapomenyana na Villa uwanjani Old Trafford.

Vijana wa Ole Gunnar Solskjaer wamezoa ushindi mara saba na kutoka sare mbili katika mechi tisa zilizopita. Hawajapoteza nyumbani Old Trafford katika mechi nne zilizopita.

Hata hivyo, Villa pia imekuwa katika hali nzuri msimu huu. Haijapoteza mechi tano zilizopita, ingawa italazimika kufanya kazi ya ziada kumaliza nuksi ya kutoshinda United katika michuano 15 zilizopita ligini.

United ikibwaga Villa itakuwa bega kwa bega na viongozi Liverpool kwa alama 33, baada ya mabingwa hao watetezi kupiga sare ya pili mfululizo walipokabwa 0-0 na wenyeji Newcastle mnamo Jumatano.

You can share this post!

‘Msoto’ watisha kuyumbisha Gor mwaka mpya ‘21

Watoto watano wafariki baada ya kutumbukia katika shimo la...