Habari Mseto

Swazuri aonywa vikali dhidi ya kuvuruga ushahidi

December 24th, 2018 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

SHIRIKA la Nation of Patriots Jumatatu limemuonya vikali aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini (NLC) Prof Muhammad Swazuri dhidi ya kuvuruga ushahidi katika kesi ya ufisadi inayomkabili mahakamani.

Wakiongozwa na kiongozi wao Bw Abdulrahman Busera, wanachama wa shirika hilo la kutetea haki za umiliki wa ardhi, walimpa Swazuri makataa ya siku saba kukoma kuingilia utendakazi wa tume hiyo.

“Iwapo Prof Swazuri hatakoma kuzima ushahidi dhidi yake, basi tutawachochea wananchi wazalendo kumkamata popote watampata na kumwasilisha kwa asasi husika,” akasema Bw Busera alipowahutubia wanahabari jijini Nairobi jana.

Shirika hilo liliwasifu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Bw Noordin Haji na Mkuu wa Idara ya Upelelezi George Kinoti kwa kupiga vita ufisadi bila ubaguzi wa kikabila.

Kiongozi wa shirika la Nation of Patriots Bw Bw Abdulrahman Busera (kati) akihutubia wanahabari jijini Nairobi Desemba 24, 2018. Picha/ Faustine Ngila

“Sisi kama wazalendo tunaunga mkono vita dhidi ya ufisadi. Lakini ulafi wa watu wachache wanaojitakia makuu unalemaza vita hivi. Hii ndio maana tunaitaka serikali kuhakikisha Prof Swazuri amefuata masharti yote ya dhamana,” wakasema.

Aidha, waliwakosoa wafisadi ambao wamekuwa wakisema kabila lao linalengwa kwenye vita dhidi ya ufisadi kwa kuwa wanapopora mali, hawafanyi hivyo kuwafaidi watu wa kabila lao bali wao wenyewe.

“Tuna hakika kwamba Prof Swazuri aliingilia ushahidi katika kesi inayomkabili ili kupunguza uzito wa kesi hiyo. Tukiitwa kutoa ushahidi kuhusu suala hili tutautoa bila wasiwasi wala uoga,” akasema Bw Busera.

Walitoa wito kwa Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) kuchunguza madai kuwa stakabadhi za ushahidi dhidi ya Prof Swazuri zilivurugwa, ndani ya NLC.

Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa tume hiyo Bi Abigael Mbagaya Mukolwe aliteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti wa tume hiyo Agosti 16 baada ya Prof Swazuri kuvuliwa mamlaka.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa NLC alifikishwa mahakamani mwezi huo akikabiliwa na mashtaka ya ufisadi kuhusiana na ulipaji wa fidia kwa ardhi kulikojengwa reli ya kisasa (SGR) ya Sh221 milioni.

Aliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kusomewa mashtaka akiwa pamoja na afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Tom Aziz Chavangi.