Habari

Swazuri atiwa nguvuni kuhusiana na sakata ya mamilioni SGR

August 11th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) Mohammed Swazuri amekamatwa Jumamosi asubuhi dakika chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noodin Haji kusema ana kesi ya kujibu kufuatia sakata ya ulipaji ridhaa kwa ardhi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Kupitia ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter, Bw Haji alisema Swazuri, naibu wake Abigael Mbagaya, Afisa Mkuu wa NLC Tom Chavangi na Mkuregenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini (KR)  Atanas Maina wanafaa kukamatwa kutokana na sakata ya ulipaji wa Sh519 milioni, kama fidia kwa ardhi ambayo serikali ilitwaa kisheria kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) eneo la Pwani Joseph Ng’ang’a alithibitisha kuwa Dkt Swazuri alikamatwa katika kaunti ya Kwale, lakini akadinda kutoa maelezo zaidi.

Lakini duru kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na DPP zilisema kuwa Swazuri, Mbagaya, Chivangi na Maina walikamatwa jijini Nairobi.

Kukamatwa kwa Swazuri ni kilele cha uchunguzi ambao umekuwa ukiendeshwa kuhusiana na sakata ya ulipaji ridhaa kwa watu ambao ardhi yao ilitwaliwa kwa ajili ya Ujenzi wa SGR.

Mwezi Julai, Seneta wa Mombasa Mohammed Faki aliwasilisha malalamishi katika bunge la seneti kwa niaba ya wakazi kadhaa wa Mombasa ambao ardhi yao ilitwaliwa lakini hawajalipwa fidia hadi wakati huu.

Watu hao wamekuwa wakielekeza kidole cha lawama kwa Dkt Swazuri na shirika la Reli Nchini kupitia Mkurugenzi wake Bw Maina.