Kimataifa

Taabani kwa kulazimisha watoto kula sabuni ili 'waoshe dhambi'

February 6th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

BABA mmoja kutoka Marekani alifunguliwa mashtaka ya kuwatesa watoto, baada ya kuwalazimisha wanawe kufanya mazoezi (push-ups) kwa dakika 30 na kula sabuni kuosha dhambi zao, walipovunja sheria za boma.

Baba huyo kwa jina James Pal wa miaka 40 aidha anadaiwa kuwalazimisha watoto hao kuosha ukuta kwa kutumia sehemu ya mbele ya kichwa kwa dakika 30, huku wakiwa wamesimama hatua mbili kutoka kwenye ukuta.

Watoto waliokuwa wakipewa adhabu hizi ni wa umri wa miaka 11 na 13, na waliripotiwa kujeruhiwa mwilini baada ya mates ohayo.

Adhabu hizi zilisemekana kuwa zilitokana na hali ya watoto hao kutomheshimu baba huyo, ndipo akapandwa na mori na kuamua kuwarudi, shirika moja la habari likaripoti.

Vilevile alidaiwa kumpiga ngumi mtoto mmoja hadi akamwacha na jeraha baya kifuani.

Mtoto mwingine naye aliachwa na mdomo uliokuwa ukiwasha na kuuma, baada ya kulazimishwa kula sabuni na mzee huyo.

Visa hivi vilitokea eneo la Mount Vernon kwa muda wa siku tano wiki iliyopita.

Mzee huyo alikamatwa Jumatatu wiki iliyopita, baada ya maafisa wa polisi kufika kuwaokoa watoto hao.