Habari Mseto

Taahira aponea baada ya ambulansi aliyoendesha kugongana na lori

March 25th, 2020 2 min read

JEREMIAH KIPLAGAT na STANLEY KIMUGE

MGONJWA wa akili Jumanne alijeruhiwa vibaya alipoamua kuendesha ambulansi kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, iliyogongana na lori la kusafirisha mafuta eneo la Marura kwenye barabara ya Eldoret-Iten.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye ni mkazi wa Kapseret, alikuwa amepelekwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.

Lakini aliwashangaza wengi alipochomoka kutoka hospitali hiyo na kuingia kwa ambulansi tukio ambalo nusura limsababishie mauti.

Polisi walimwandama, baada ya kupashwa habari kuhusu kisa hicho na wakampata amejeruhiwa baada ya ajali hiyo kutokea katika eneo la Marura, katika barabara ya Eldoret-Iten.

Mgonjwa huyo alipata majeraha mabaya kichwani lakini dereva wa lori hilo alipata majeraha madogo. Alikwepa kugonga matatu mbili za abiria 14 kabla ya kugonga lori hilo la mafuta.

Afisa Mkuu Mtendaji katika hospitali hiyo, Bw Wilson Aruasa alisema mwanamume huyo alikuwa akihudumiwa na mhudumu mmoja wa afya alipochomoka na kuangia ndani ya ambulansi na kuiendesha kwa kasi.

Ilisadifu kuwa ambulansi hiyo ambayo ni mali ya kituo cha afya cha Kaptendon, Kapseret, Uasin Gishu, ilikuwa na ufunguo.

“Dereva hakuwa amezima ambulansi hiyo. Mwanamume huyo aliingia ndani ya gari na kuchomoka nalo,” Dkt Aruasa akaambia Taifa Leo.

Afisa huyo alisema mwanamume huo aliwahi kupewa matibabu katika hospitali hiyo hapo awali ambapo alidhihirisha sifa zinazofanana na wagonjwa wenye akili punguani.

Dkt Aruasa alisema dereva wa ambulansi hiyo alikuwa ameiegesha karibu na kitengo cha shughuli za dharura na alikuwa akimsaidia muuguzi kumpeleka mgonjwa mwingine katika chumba cha dharura.“Huyu ni mtu anaugua ugonjwa wa kiakili.

Dereva ameagizwa aandikishe taarifa kwa sasa hiki ni kisa cha kushughulikiwa na polisi,” akaongeza Dkt Aruasa.

Eneo la kuingilia katika kitengo cha kushughulikia ajali na dharura nyinginezo ni wazi na halina lango. Kitengo hicho kiko karibu na barabara ya Nandi inayounganisha hospitali ya MTRH na eneo la katikati mwa mji wa Eldoret.Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) kaunti ndogo ya Turbo Eliud Maiyo alisema mgonjwa huyo anapokea matibabu.

“Alitwaa udhibiti wa ambulansi hiyo dakika chache baada ya mgonjwa mwingine kuondolewa na akaliendesha kwa kasi mno. Alipata majeraha na akakimbizwa hospitalini ambako anapewa matibabu ya dharura,” Bw Maiyo akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Bw Ambrose Lagat, aliyeshuhudia kisa hicho, alituambia kwamba mwanamume huyo alikuwa akiliendesha ambulansi kwa kasi na katika safu ya barabara isiyokubalika.

Ndio maana wenye magari walikwepa barabara kukwepa kugongana na ambulansi hiyo.

“Tulishangaa kuwa ambulansi hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi na haikupiga king’ora kuonya magari mengine yaipishe. Iligonga vioo ya pembeni vya matatu mbili kabla ya kugongana na lori la mafuta upande wa kulia,” akasema.

Baada ya mgangano huo, lori la mafuta lilianguka barabarani na kuiziba, na kusababisha msongamano wa magari katika barabara yenye shughuli nyingi.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kudhibiti umati wa watu waliofika eneo hilo la ajali. Maafisa hao waliwazuia kufyonza mafuta kutoka kwa lori hilo.