Makala

Taasisi ya kozi za ufundi ya miaka 99 ambayo ilikuwa gereza wakati wa utawala wa mkoloni

June 26th, 2020 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

[email protected]

TAASISI ya kozi za ufundi ya Kigumo katika Kaunti ya Murang’a iko na historia ya kipekee kwa kuwa majengo yake yamedumu miaka 99 sasa na mashujaa katika vita vya kusaka uhuru wa taifa hili walikuwa wakifungwa na wakoloni katika taasisi hiyo.

Kati ya 1952 na 1960 wapiganiaji uhuru walionaswa na kuhukumiwa kama ‘magaidi’ walikuwa wakihudumu vifungo vyao katika gereza hili ambalo kwa sasa huwahami vijana na kozi za ufundi.

Majengo yenyewe yamedumu tangu 1920 na kwa kawaida, yamedhoofika kiasi kwamba yanatoa taswira ya kuhitaji tu uchochezi mdogo wa msukumo wa kimazingira na yaporomoke.

Wapenda maendeleo katika eneo hili waliketi chini mwaka wa 1990 kujadili kuhusu majengo haya na ikawa bayana kuwa yalifaa yabomolewe kwa kuwa hata simiti ya kuunganisha jointi zake ilikuwa imeishiwa na makali.

Ni majengo ambayo yalionekana kuwa hatari kwa makazi au matumizi ya binadamu lakini wazo likatolewa kuwa badala ya kuharibu majengo hayo yenye umuhimu mkuu kwa historia ya taifa hili, yageuzwe kuwa ya manufaa na ustawi wa kijamii.

“Ndipo yakageuzwa kuwa pahala pa kuwahami raia na kozi za ufundi ili wawe na mashiko ya kiuchumi ya kujitafutia riziki,” asema Mzee James Wachie, 89.

Majengo hayo yenye seli 36 ambazo sasa baadhi yazo ndizo hutumika kama madarasa na maabara pamoja na afisi za wakufunzi, yalikuwa yakilengwa yasukumiwe viongozi wa eneo hilo watoe pesa za kuyajenga upya na kuimarisha taasisi hiyo, aongeza.

Lakini tangu mwaka huo wa 1990, hakuna ufadhili ambao umetolewa wa kukarabati majengo na kuyageuza ya kisasa, hii ikiwa ndiyo hali ambayo naibu wa waziri wa Elimu Zack Kinuthia alikumbana nayo Alhamisi katika ziara yake ya kikazi.

Kutoka Kushoto: Meneja wa taasisi ya kozi za ufundi ya Kigumo, John Mbote, mkurugenzi wa elimu za kozi za ufundi hapa nchini Bw Mutinda Mwaa na Waziri Msaidizi wa Elimu Zack Kinuthia. Picha/ Mwangi Muiruri

Ni taasisi ambayo kikatiba iko chini ya uratibu wa serikali ya Kaunti ya Murang’a lakini katika ule umoja wa utawala, Bw Kinuthia akasaka maelewano na Kaunti ili kuwa na mkataba wa kusaidia taasisi hiyo ijipe umbo wa kisasa.

“Sisi kama serikali kuu ndio hufadhili elimu ya kozi za ufundi na huwa tunatoa Sh15,000 kwa kila mwanafunzi ambaye hujiunga na taasisi hizi zilizo chini ya uratibu wa kaunti. Hii ina maana kuwa kozi hizo hutolewa bila malipo,” asema.

Alisema kuwa serikali za Kaunti nazo zimewajibishwa na ujenzi na utoaji wa vifaa kwa wanafunzi.

Taasisi hii ya Kigumo ikiwa katika kipande cha ardhi ukubwa wa ekari tatu inatajwa na Mzee Joram Thumbi 86 kama “inayonikumbusha harakati za kusaka uhuru wetu ambapo damu, machozi na jasho lilitutoka.”

Anasema kuwa kila wakati angesikia milio ya risasi kutoka taasisi hii katika enzi hizo za kuwa gereza, alikuwa aking’amua tu kwamba aidha kuna uvamizi wa mashujaa wa Maumau wakilenga kuwanusuru wafungwa, au kuna wafungwa waliokuwa katika harakati za kutoroka na maaskari wa kikoloni walikuwa wakiwalenga kwa risasi kutoka kijichumba kidogo juu ya majengo hayo cha kuthibitia usalama wa gereza hilo.

“Naibu waziri Kinuthia ambaye ni mtoto wetu wa kutoka hapa Kigumo karibu katika taasisi hii yenye umuhimu mkuu kwa hisia na historia ya wenyeji… Hili ni kama kasiri la kumbukumbu za Maumau,” Naibu kamishna wa Kigumo, Margaret Mbugua akamkaribisha mgeni wa heshima.

Alisema kuwa taasisi hiyo inafaa kuundwa upya na kuwe na uhamasisho wa kijamii ili wale wote ambao hawana ujuzi wa kozi eneo hilo wasajiliwe na wapate masomo bila kutoa hata ndururu.

Meneja wa taasisi hiyo John Mbote alisema atahitaji bajeti ya Sh50 milioni kuzindua ujenzi wa jengo la kisasa ili kuipa sura ya kupendeza na kutoa umbo wa kuvutia vijana wajisajili kama wanafunzi.

‘Kwa sasa tuko na wanafuzni 68 ambao wanajipa kozi za ujenzi, urembo, chakula na teknolojia za mapishi na ushonaji nguo. Tukipata ufadhili wa kutosha, tunaweza tukapanua uwezo wetu wa kozi hadi nyanja 15 na tuwe na wanafunzi zaidi ya 200 katika kila awamu ya usajili,” akasema.

Bw Kinuthia alisema kuwa atamwandama rais Uhuru Kenyatta ili awatafutie wenyeji usaidizi wa kifedha wa kuimarisha taasisi hiyo.

“Rais akiwa mwana wa mwanzilishi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta na ambaye alikuwa katika harakati za kupigania uhuru wa taifa bila shaka ataguswa na malilio yenu ya ufadhili,” akasema.

Lakini kabla ya hayo kufanyika, mkurugenzi wa elimu za kozi za ufundi hapa nchini Bw Mutinda Mwaa alisema kuwa ana mbinu ya kutoa afueni ya muda kwa taasisi hiyo.

“Mimi ndiye hugawa pesa za kugharimia elimu katika taasisi hizi. Ikiwa mtapata usajili wa wanafunzi wengi, mimi nitatuma pesa nyingi kwenu. Fanya hesabu: Kwa kila mwanafunzi huwa ninatuma Sh15,000. Mkiwa na wanafunzi wengi, nitatuma pesa nyingi; sajilini wengi niwape pesa,” akasema.

Alisema kuwa ni aibu kuwa miaka 57 baada ya uhuru kupatikana, taasisi kama hiyo iliyo na umuhimu mkuu wa kuwa hifadhi ya kihistoria imekumbwa na matatizo ya ufadhili.