HabariSiasa

Tabia ya Sonko kurekodi watu ni ushenzi, nitamkomesha – Kang'ata

June 9th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a, Irungu Kang’ata Jumapili amesema kuwa atawasilisha hoja katika bunge la Seneti ya kushinikiza gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko aorodheshwe kama hatari kwa usalama wa kitaifa.

Alisema msingi wa hoja hiyo utakuwa tabia ya Sonko ya kurekodi maongezi yake ya simu na viongozi wengine na kisha kuanika kanda hizo katika mitandao ya kijamii.

“Hivi majuzi ameanika maongezi yake ya siri na Mwakilishi Mwanamke wa Nairobi Bi Esther Passaris na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu wakishauriana jinsi ya kutatua shida ya mkewe Waititu (Susan Wangare) ya kutiwa mbaroni na askari wa jiji kwa tuhuma za kujenga bila idhini,” akasema.

Alisema kuwa kuna wakati mwingine ambapo Sonko alimpigia simu Rais Uhuru Kenyatta akiwa katika mtaa wa South C ambapo alikuwa akisaka usaidizi wa Ikulu mijengo iliyosemwa kujengwa kwa idhini haramu ikome kubomolewa.

“Aliishia kuanika maongezi hayo katika mitandao ya kijamii na pia kumwangazia rais kama aliyekuwa akifuata sheria kwa njia ya mkato kwa kunusuru waliokuwa hatiani,” akasema.

Kang’ata alisema kuwa “tabia hii ya Sonko kwanza ni kinyume na sheria kwa kuwa hakuna aliye na idhini ya kunakili maongezi ya kibinafsi ya simu.”

Aidha, alisema kuwa Sonko ako katika hali nzuri ya kuwa akiongea na viongozi wengi tajika akiwa ni Gavana ambaye pia amewahi kuhudumu kama Seneta na mbunge.

“Huwezi ukajua ni siri ngapi amejiwekea za maongezi ya simu na viongozi. Huwezi jua athari za siri hizo kwa usalama wa kitaifa. Huwezi ukajua atalenga kuachilia maongezi hayo lini kukiwa na hali gani katika taifa hili.

“Ndiyo sababu nalenga siri hizo zidunishwe na hali rasmi ya yeye kuorodheshwa kama hatari kwa taifa na asiye wa kutegemewa katika ufichuzi wake wowote wa baadaye. Huo ni ushenzi,” akasema.

Alisema bunge la Seneti liko na na mamlaka sawa na Mahakama kuu na ambapo uamuzi huo ukiafikiwa, basi utakuwa uamuzi halali wa kuorodheshwa kama hukumu dhidi ya Sonko.