Habari

Tabichi awapa walimu Uingereza mbinu za kufundisha

October 3rd, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

MWALIMU Peter Tabichi, aliyeshinda tuzo ya Mwalimu Bora Duniani mwaka huu, ametoa ushauri kwa walimu nchini Uingereza kuhusu mbinu za kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi.

Alitoa ushauri huo kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika jana katika Makavazi ya Sayansi, jijini London, ambako alikutana na walimu wa masomo hayo nchini humo.

Akihutubu kwenye kikao hicho, Bw Tabichi alieleza jinsi alikuza Klabu cha Somo la Sayansi katika Shule ya Upili ya Kiriko, Kaunti ya Nakuru, ambako anafunza.

Kwenye kikao hicho, kilichoandaliwa na Kundi Maalum la Masomo ya Sayansi la Uingereza, Bw Tabichi alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wazazi na wanafunzi ili kuwaeleza kwa undani kuhusu umuhimu wa kundi hilo. Alisema ni ushirikishi huo ambao uliwasaidia wanafunzi kuimarisha matokeo katika masomo hayo, ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa magumu.

“Ninapowafunza wanafunzi wangu kuhusu dunia na vile inavyoendelea, huwa ninaona wanavyofurahia. Hivyo ndivyo nilifurahia nilipoona jinsi wadau mbalimbali walijitolea katika kikao hiki. Lazima tufahamu kuwa njia kuu ya kupata mafanikio kwenye ufunzaji wa sayansi ni kupitia mbinu tekelezi,” akasema Bw Tabichi.

Kundi hilo huwa linaandaa vikao kama hivyo ambapo walimu wa masomo ya Sayansi kama Bayolojia, Fizikia na Kemia hupata nafasi kubadilishana mawazo kuhusu mbinu za kuimarisha ufunzaji wake.

Licha ya ushindi wake, nchi nyingi za Afrika bado zinakumbwa na changamoto nyingi kuhusu mifumo ya ufunzaji wa masomo ya sayansi.

Hata hivyo, alieleza kuwa ana imani kuwa Afrika inaweza kuepuka changamoto hizo, kwa kutilia mkazo uondoaji dhana kuwa masomo hayo ni magumu.

“Ninaamini Afrika ikiwa na uwezo mkubwa wa kielimu kama Uingereza, inaweza kutoa wanasayansi maarufu ambao watachangia pakubwa kwenye maendeleo duniani,” akasema. Mkurugenzi wa kundi hilo Bi Susan Raikes alieleza furaha yake, akisema kuwa walifaidika kutokana na ushauri huo.