Habari Mseto

Tafadhali msitafune mabilioni ya Hazina ya Covid-19 – Rais Kenyatta

April 17th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameonya dhidi ya matumizi mabaya au ufujaji wa fedha za Hazina ya Dharura ya Kusaidia waathiriwa wa ugonjwa wa Covid-19.

Kwenye hotuba yake kwa taifa Alhamisi, Rais Kenyatta alifichua kuwa kufikia sasa hazina hiyo imepokea jumla ya Sh1 bilioni, pesa ambazo zitatumika kufadhili mpango wa kuwasambazia vyakula vya msaada watu kutoka jamii masikini.

“Taifa letu linaongozwa na watu wenye huruma na upendo. Hii ndio maana tunaendesha mpango wa kuwasambazia wale walioathirika zaidi chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Pia, tumeanzisha Hazina maalum ambayo kufikia sasa imepokea zaidi ya Sh1 bilioni, ambazo zinapasa kutumiwa kuwafaidi walengwa,” akasema.

Rais Kenyatta alisema ikiwa pesa za hazina hizo zitatumiwa vizuri, zitaweza kuzifaa familia mbalimbali ambazo zimeathirika na janga hili.

“Hii ndio maana ninasisitiza kuwa fedha hizi na zingine ambazo zitaelekezwa katika Hazina hii zinapasa kutumika kwa ungalifu mkubwa. Huu ni wakati wa kuwasaidia raia wetu wasiojiweza wala sio nafasi ya watu fulani kufuja pesa hizo,” akafafanua alipohutubu kutoka Ikulu ya Nairobi.

Alisema michango yote ya kuwasaidia waathiriwa wa Covid-19 inapasa kuelekezwa katika Hazina hii, kiongozi wa taifa akashauri.

Rais Kenyatta alisema utawala wake umetambua familia zenye mahitaji katika kaunti ya Nairobi ambazo zitafaidi kutokana na mpango wa serikali ya kusambaza vyakula na fedha za matumizi mara moja kila wiki.

Aliongeza kuwa serikali kuu imetoa Sh5 bilioni kupiga jeki juhudi za serikali za kaunti ya kuwasaidia Wakenya waliathirika na maambukizi ya virusi vya corona.

“Pesa hizi zinapasa kutumika kununua vifaa vya kujikinga, kama vile maski, ambavyo vinapasa kusambazwa bila malipo kwa wananchi.,” Rais Kenyatta akasema.

Aliongeza kuwa serikali imetoa Sh8 bilioni zingine za kufadhili mpango wa serikali wa kuwasaidia wakongwe.