• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Badminton Kenya yapigwa marufuku baada ya mivutano ya uongozi ya miaka minne

Badminton Kenya yapigwa marufuku baada ya mivutano ya uongozi ya miaka minne

Na AYUMBA AYODI

SHIRIKISHO la mchezo wa badminton duniani (BWF) limepiga marufuku Kenya.

Katika taarifa yake mnamo Machi 9, katibu mkuu wa BWF Thomas Lund alifichua kuwa marufuku hiyo ya muda usiojulikana utadumu hadi pale migogoro katika Shirikisho la Mchezo wa Badminton nchini Kenya (BK) itakaposuluhishwa kupitia kuandaa uchaguzi wa huru na wazi inavyohitajika na BWF.

Aliongeza kuwa, katika barua ya Machi 9 mwaka 2021 kwa mirengo inayoongozwa na Peter Muchiri na Geoffrey Shigoli, zoezi hilo litahitaji kuidhinishwa katika mkutano wa kila mwaka wa BWF mnao Mei 22 mwaka huu.

BK ni shirikisho la pili Kenya kupigwa marufuku kutokana na mivutano ya uongozi baada ya Shirikisho la Uogeleaji mwaka 2020.

“Kwa mujibu wa katiba ya BWF kifungu 5.5 na 13.5, kikao cha BWF kimeamua kusimamisha uanachama wa Badminton Kenya,” alieleza Lund na kuongeza kuwa kutokana na marufuku hiyo, Badminton Kenya itanyimwa haki ya kupiga kura katika mikutano ya BWF, kupokea ufadhili ama usaidizi wowote wa kifedha, na kuingiza wachezaji moja kwa moja katika mashindano.

Lund alisema katika barua hiyo iliyotumiwa pia rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Paul Tergat na rais wa BWF Poul-Erik Hoyer kuwa japo kundi la Shigoli linatambuliwa na BWF, marufuku hiyo inaenda kwa mtu yeyote anayewakilisha Kenya katika mchezo wa badminton.

Lund alisema kuwa suluhu yoyote itakayofikiwa lazima ilete pamoja pande hizo tofauti ndiposa ikubaliwe na BWF.

“Ingawa tunajuta kuchukua hatua hiyo muhimu, tuko tayari kuingilia kati kusaidia pande hizo bila ya kupendelea yeyote na kuandika makubaliano yatakayofikia uchaguzi ambao hautagawanya shirikisho,” alisema Lund na kuongeza kuwa wanasubiri kufikiwa na pande husika.

Lund alisema kikao cha BWF kililazimika kuchukua adhabu hiyo kali kwa sababu migogoro hiyo imedumu kwa karibu miaka minne na hakuna dalili kuwa suluhisho inatafutwa.

“Hii inaenda kinyume na kifungu cha 5.4 cha katiba ya BWF ambacho kinahitaji kuwepo kwa mfumo mzuri wa kuchagua viongozi,” alisema Lund.

Alieleza kuwa mnamo Januari 4 waliipa BK makataa ya Februari 7 mwaka huu wa 2021 ifanye uchaguzi utakaoleta wote pamoja, wa haki na wazi.

“Tuliongeza makataa baada ya NOC-K kujitolea kusuluhisha tofauti hizo,” alisema Lund. “Kwa bahati mbaya, licha ya pande hizo kukutana mara mbili kabla ya siku hiyo ya mwisho, hatujapiga hatua ya maana kuhusu uchaguzi mpya.”

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Bandari yafurahia uteuzi wa wachezaji wake wawili...

Marejeo ya Fabinho yatatupiga jeki katika gozi la UEFA...