• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Cindy asimulia changamoto zinazowakumba waigizaji, mastaa

Cindy asimulia changamoto zinazowakumba waigizaji, mastaa

Na JOHN KIMWERE

MWANZO wa ngoma kila mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia.

Ni katika kutumainia na kuvumilia ambapo ana imani ipo siku nyota yake itang’aa na kuibuka msanii wa kimataifa.

Galia Cynthia Sylvia maarufu Cindy ni kati ya wana maigizo wanaokuja wakilenga kujituma mithili ya mchwa ili kufikia upeo wa juu.

Kando na uigizaji kisura huyu ni mtangazaji wa redio ya mtandaoni (online) pia ni mratibu wa sherehe (MC).

Binti huyu anasema hakufahamu kuwa angejiunga na masuala ya uigizaji alianza tangia akiwa Shule ya Msingi.

”Tangu utotoni mwangu nilidhamiria kuhitimu kuwa mtangazaji ambapo kwa asilimia fulani ndoto yangu inaelekea kutimia,” anasema na kuongeza kuwa ana imani milango itafunguka na kutinga kiwango anacholenga.

Dry Spell

Katika mpango mzima kisura huyu anasema kuwa angependa kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kutoa ajira kwa waigizaji wanaoibukia.

Pia anataka kuwa kati ya waelekezi wazuri katika shughuli za kuzalisha filamu nchini.

”Sijapata mashiko katika tasnia ya uigizaji lakini nimefahamu mengi ambapo nimegundua tunapaswa kushikana mikono pia kuwa na ushirikiano kwa kufanya kazi nzuri,” akasema.

Anasema anatamani sana kuona ndoto yake ikiendelea kutimia ikiwamo kushiriki filamu na zipate mpenyo kupeperushwa kwenye runinga.

Galia Cynthia Sylvia maarufu Cindy msanii anayekuja katika sekta ya maigizo. PICHA | JOHN KIMWERE

Ingawa hajapiga hatua katika maigizo anajivunia kufanya kazi na makundi kama More Media ‘Love Me’, ‘Dry Spell,’ pia Vijana Hodari ambapo wamefanya michezo ya kuigiza wakifuata mwongozo wa vitabu vya kutahiniwa shuleni (setbooks).

Anasema hapa Afrika angependa kufanya kazi na Elizabeth Michaels maarufu Lulu ambaye ni Mtanzania anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Chumvi’ na ‘Majizo Athibitisha’ kati ya nyingine.

Ushauri

Anahimiza wenzie wajitume bila kulegeza kamba nyakati zote wanapopata nafasi kuonyesha talanta zao iwe katika uigizaji ama taaluma nyingine. Anadokeza kuwa serikali inapaswa kuweka mbinu mwafaka kuhakikisha waigizaji wanaendeleza shughuli zao bila vikwazo maana zipo sheria zinazowazuia. Anashikilia kuwa sheria zingine zimezima juhudi za wasanii wengi wanaokuja kufanya kazi ya uigizaji.

Pandashuka

Anasisitiza kuwa sekta ya uigizaji imejaa milima na mabonde.

”Kiukweli baadhi ya maprodusa huomba kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na waigizaji wa kike ili kuwapa ajira,” anasema na kutoa wito kwa wenzie kuwapigia chini maprodusa sampuli hiyo.

Anasema kuwa pia ulingo wa burudani umejaa matapeli wengi ambao mara nyingi huponda wasanii wapya kwenye gemu.

”Pia siwezi kuweka katika kaburi la sahau visa vya makundi mengine kuvunjika na kujikuta bila ajira. Mara nyingi masuala ya uongozi na mapato ndio huchangia makundi mengine kusambaratika,” akasema.

Anasema taifa hili limefurika waigizaji chipukizi wanaopania kuibuka watajika miaka ijayo.

You can share this post!

Wakulima wa Kiambu wahimizwa kupanda miparachichi na...

UCHAMBUZI WA FASIHI: Wahusika, maudhui na vitushi: Sura ya...

T L