• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Dandora Youth FC yadhaminiwa kwa Sh2 milioni

Dandora Youth FC yadhaminiwa kwa Sh2 milioni

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Dandora Youth kutoka ligi ya daraja ya tano ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF), imejawa motisha ya kutafuta kupandishwa daraja hadi Ligi Kuu baada ya kupigwa jeki kwa Sh2 milioni na Skyward Express kupitia ushirikiano wa kampuni hiyo ya ndege na wakfu wa mwanasoka Johanna Omolo.

Katika kikao na wanahabari katika afisi ya kampuni hiyo katika uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi, Kocha Ezekiel Akwana na nahodha Brian Chege walisema kuwa udhamini huo utasaidia pakubwa katika kupunguza changomoto klabu hiyo inapitia na kuiwezesha kumakinikia uwindaji wa kupanda ngazi.

“Naamini matokeo yetu yataimarika kuanzia mechi yetu ya kwanza ya mkondo wa pili dhidi ya Wajiji hapo Agosti 7,” alisema Chege.

“Udhamini huu ni motisha tosha sisi kujituma vilivyo kukwea ngazi ya ligi tunayoshiriki na kufika Ligi Kuu. Tupe misimu minne ijayo, tutakuwa mbali,” alisema mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Akwana.

Omolo, 31, ambaye ana uraia wa Ubelgiji baada ya kuchezea CS Vise, Beerschot, Lommel, Royal Antwerp na Cercle Brugge nchini humo kati ya Julai 2007 na Desemba 2020, alieleza furaha yake katika ushirikiano huo.

“Dandora Youth ni timu ya mtaa kwa hivyo udhamini huu ni muhimu umewasili wakati unaofaa. Naamini utasaidia katika kukuza na kuinua talanta,” alisema Omolo ambaye msimu uliopita alichezea Buyuksehir Belediye Erzurumspor nchini Uturuki.

Mwenyekiti Mohamed Abdi alisema ushirikiano huo ni wa miaka miwili, ingawa akafafanua kuwa kuna uwezekano wa kuuongeza.

“Kupitia ushirikiano huu, Dandora Youth itapokea Sh2 milioni kila mwaka,” alisema Abdi na kufichua kuwa amekuwa akisaidia timu hiyo, japo kwa kiasi kidogo “kwa sababu ya kuvutiwa nayo kupitia rafiki ambao walifanya nipate kumjua nyota Johanna Omolo”.

Vijana wa Akwana, ambaye aliwahi kuwa kocha mkuu wa Sofapaka kwenye Ligi Kuu, hutumia uwanja Tom Mboya mtaani Dandora kwa mechi zake za nyumbani. Klabu hiyo inashikilia nafasi ya nne katika ligi ya FKF ya kaunti ya Nairobi kwa alama 20 baada ya kujibwaga uwanjani mara 13.

You can share this post!

Dhuluma za kisaikolojia zinavyawatesa wanandoa kipindi cha...

Hatimaye Kenya yashinda dhahabu ya kwanza Olimpiki