• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Der Klassiker: Mwanzo mzuri Thomas Tuchel akisajili ushindi

Der Klassiker: Mwanzo mzuri Thomas Tuchel akisajili ushindi

Na MASHIRIKA

THOMAS Tuchel alianza safari yake ya ukufunzi kambini mwa Bayern Munich kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya waajiri wake wa zamani Borussia Dortmund katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ugani Allianz Arena, Jumamosi.

Mabao ya Bayern yalijazwa kimiani kupitia kwa Thomas Muller (mawili), Kingsley Coman na kipa Gregor Kobel wa Dortmund aliyejifunga. Emre Can alifunga penalti kabla Donyell Malen kuwapa Dortmund bao la pili.

Muller sasa anajivunia kufunga mabao saba katika gozi la Der Klassiker kati ya Bayern na Dortmund. Ni wanasoka watatu pekee wamewahi kufunga magoli zaidi ya hayo katika historia ya kipute hicho.

Bao la Coman lilikuwa la 40 kwa Bayern kufunga Dortmund katika Bundesliga chini ya misimu sita iliyopita. Mabingwa hao watetezi sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 55, mbili kuliko nambari mbili Dortmun ambao pia wametandaza mechi 26.

Ushindi wa Bayern wanaowania taji la Bundesliga kwa mara ya 11 ulikomesha rekodi ya kutopigwa kwa Dortmund katika mechi 10 mfululizo za ligi mwaka huu.

Bayern wangalijivunia ushindi mnono zaidi ila magoli ya Eric Maxim Choupo-Moting na Serge Gnabry yakafutiliwa mbali baada ya kubainika kuwa walicheka na nyavu za wageni wao wakiwa wameotea.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Tuchel kusimamia kambini mwa Bayern waliomtimua kocha Julian Nagelsmann mwishoni mwa mwezi jana baada ya Dortmund kuwapita kileleni mwa jedwali. Tuchel aliwahi kudhibiti mikoba ya Dortmund kati ya 2015 na 2017.

Baada ya kung’oa Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa jumla ya mabao 3-0 msimu huu, Bayern sasa wana kibarua kizito cha kudengua Manchester City kwenye robo-fainali.

Watapania kutegemea zaidi maarifa ya Tuchel aliyeongoza Chelsea kukomoa Man-City 1-0 kwenye fainali ya UEFA 2021 jijini Porto, Ureno. Tuchel, 49, alipigwa kalamu na Chelsea mnamo Septemba 2022 baada ya msururu wa matokeo duni.

Aliwahi pia kunoa PSG kati ya 2018 na 2020 na alinyanyulia Chelsea ufalme wa UEFA mnamo Mei 2021. Taji hilo lilikuwa kati ya matatu aliyoshindia miamba hao wa Uingereza chini ya miezi 20 ugani Stamford Bridge na akatawazwa Kocha Bora wa Mwaka Duniani msimu uliofuatia.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Bayern Munich 4-2 Dortmund

Union Berlin 3-0 Stuttgart

Schalke 0-3 Bayer Leverkusen

RB Leipzig 0-3 Mainz

Freiburg 1-1 Hertha Berlin

Wolfsburg 2-2 Augsburg

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Arsenal hawashikiki vitani EPL

Chelsea wampiga kalamu kocha Graham Potter

T L