• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Ghost Mulee akwama India baada ya Kenya kusimamisha safari za ndege

Ghost Mulee akwama India baada ya Kenya kusimamisha safari za ndege

Na DAVID KWALIMWA

KOCHA wa Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee ni mmoja wa Wakenya waliokwama nchini India kufuatia tangazo la serikali kusimamisha safari za ndege kutoka na kuingia nchini kutoka taifa hilo.

Mulee, 53, na kakake wamekuwa wakipokea matibabu katika hospitali ya Apollo jijini New Delhi kwa majuma matatu yaliyopita.

“Nashukuru Mungu kuwa tumepona na tunashukuru Wakenya kwa usaidizi wao na maombi,” alisema kupitia njia ya simu kutoka India mnamo Alhamisi.

“Madaktari wameturuhusu tuondoke hospitali na tumewasiliana na ubalozi wa Kenya hapa tukisubiri Waziri wa Afya Mutahi Kagwe atangaze mipango ya usafiri ili tuweze kurejea nyumbani.”

Juma lililopita, Kagwe alitangaza kusimamisha safari za ndege kutoka India kwa siku 14 kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Pia, alitangaza kuwa wasafiri wanaopitia India kuja Kenya lazima waingie karantini siku 14 ambayo itakuwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya.

Mulee alisisitiza kuwa yuko fiti na tayari kuongoza Kenya katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022.

Mechi hizo za kuelekea nchini Qatar mwaka 2022 zilikuwa zimepangiwa kuanza mwezi ujao (Juni), lakini zimeahirishwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) hadi Oktoba kutokana na changamoto zinazosababishwa na janga la corona.

“Ni habari njema (kuwa mechi za kufuzu zimesukumwa mbele),” alisema Mulee.

“Wachezaji wetu wengi wanaocheza nyumbani hawajakuwa na mashindano na nilikuwa na hofu kuhusu usawa wao kimwili kabla ya mechi hizo muhimu. Tuko pabaya. Tulikuwa na changamoto hii dhidi ya Comoros mwaka jana na iliathiri mchezo wetu. Kupanguliwa kwa mechi za Juni kunanipa muda mzuri wa kuwaangalia na kupanga vyema.”

Mulee pia alisifu hatua ya CAF kutunga masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kwa timu zote na wachezaji.

“Katika mechi zetu zilizopita dhidi ya Comoros na Togo, tulitoka Nairobi wachezaji wetu wote wakiwa wamepita vipimo vya virusi vya corona. Tulipowasili katika mataifa hayo, tuliambiwa kuwa baadhi ya wachezaji wetu walifeli vipimo hivyo. Walipopimwa baada ya kurejea nchini, hawakupatikana na virusi hivyo. Nafurahi kuwa CAF inatunga sheria za kusimamia upimaji wa timu.”

Kenya inatafuta kuingia Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake. Imekutanishwa na Uganda, Rwanda na Mali.

Mnamo Alhamisi, CAF ilithibitisha mabadiliko hayo kupitia taarifa ikiyataja kuwa yalisababishwa na janga la virusi vya corona.

Mechi hizo za kufuzu sasa zitafanyika miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba 2021 na Machi 2022.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

AKILIMALI: Kwa mtaji wa Sh40,000 pekee wanahesabu maelfu...

Safari Rally kuwa na helikopta15, helipadi kuundwa