• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Haaland abadilishana jezi na refa anayestaafu baada ya kuongoza Dortmund kuzamisha Leverkusen ligini

Haaland abadilishana jezi na refa anayestaafu baada ya kuongoza Dortmund kuzamisha Leverkusen ligini

Na MASHIRIKA

FOWADI Erling Braut Haaland alifunga mabao mawili dhidi ya Bayer Leverkusen na kusaidia waajiri wake Borussia Dortmund kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa matao ya juu.

Ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na Dortmund katika mechi hiyo iliwawezesha kumaliza kinyang’anyiro cha Bundesliga muhula huu ndani ya mduara wa tatu-bora kwa alama 64, moja nyuma ya nambari mbili RB Leipzig waliopepetwa 2-1 na Union Berlin.

Haaland alifunga magoli katika dakika ya tano na 84 na kukamilisha msimu akijivunia jumla ya mabao 47 kutokana na michuano 49 kwenye mapambano yote muhula huu katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Mwishoni mwa gozi hilo dhidi ya Leverkusen, Haaland ambaye ni raia wa Norway alibadilishana jezi na refa Manuel Grafe aliyekuwa akisimamia mchuano wake wa mwisho kabla ya kustaafu rasmi muhula huu.

Katika mechi nyingine, Cologne walifunga bao katika dakika za mwisho na kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Schalke. Ufanisi huo uliwawezesha kufuzu kwa mchujo wa kusalia Bundesliga huku Werder Bremen waliokomolewa 4-2 na Borussia Monchengladbach wakiteremshwa ngazi. Sebastiaan Bornauw alifungia Cologne bao hilo la pekee na la ushindi dhidi ya Schalke katika dakika ya 86.

Ina maana kwamba Werder waliotawazwa mabingwa wa Bundesliga mnamo 2003-04 wanashuka ngazi kutoka Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Mei 22, 2021):

Cologne 1-0 Schalke

Union Berlin 2-1 RB Leipzig

Dortmund 3-1 Leverkusen

Frankfurt 3-1 Freiburg

Bayern 5-2 Augsburg

Bremen 2-4 M’gladbach

Hoffenheim 2-1 Hertha Berlin

Stuttgart 0-2 Arminia

Wolfsburg 2-3 Mainz

You can share this post!

Lewandowski avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye...

Shughuli ya utoaji chanjo ya polio yazinduliwa Kiambu