• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Juhudi kuhifadhi na kukuza vyakula vya kiasili 

Juhudi kuhifadhi na kukuza vyakula vya kiasili 

NA SAMMY WAWERU

KENYA ni kati ya mataifa ambayo kulingana Shirika la Umoja wa Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), limehangaishwa pakubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kuanzia kiangazi, ukame, mafuriko, mkurupuko wa wadudu hatari, na magonjwa, ndio sababu wakulima wanahimizwa kukumbatia mimea inayostahimili athari hizo hasi.

Jephline Ojwan’g, mkulima kutoka Migori wakati wa Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika, katika Makavazi ya Kitaifa – Kenya akielezea kuhusu mazao asilia anayozalisha. PICHA|SAMMY WAWERU

Isitoshe, wanashauriwa kukumbatia mifumo, teknolojia na bunifu za kisasa kuboresha mazao.

Kufanikisha malengo hayo, muungano wa Inter-Sectoral Forum on Agrobiodiversity and Agroecology (ISFAA) unaoleta pamoja sekta za serikali na za kibinafsi katika kilimo, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ya utafiti, na makundi ya wakulima kwa lengo la kilimo endelevu na kuboresha mazingira, mwaka huu umeandaa Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika.

Unga unaotokana na nafaka asilia ambazo ADS – Western inahamasisha wakulima kukuza. PICHA|SAMMY WAWERU

Hafla hiyo ya wiki iliyopita na iliyofanyika katika Makavazi ya Kitaifa – Kenya, Nairobi Oktoba 11 – 12 kauli mbiu yake ilikuwa: Kuadhimisha Uhuru wa Chakula na Mbegu Nchini Kenya – Kufufua na kulinda Mfumo wetu wa Chakula na Kilimo huku tukikita Mizizi yetu, Kudumisha Mustakabali Wetu wa Kwanza.

Makala hayo ya Pili ya ISFAA, yalikusanya na kuleta pamoja wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaozalisha chakula asilia, na walitumia jukwaa hilo kuonyesha mazao na mbegu.

Karen Nekesa, mwanachama wa ISFAA akionyesha maboga asilia. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, nafaka zilikuwa kibao, kuanzia mahindi ya rangi, mseto wa maharagwe, njugu karanga za aina tofauti, wimbi, mtama, mihogo, maboga (malenge), viazi mbatata, viazi vitamu, uyoga na mbegu za mboga za kienyeji.

Jephline Ojwan’g, alikuwa miongoni mwa washirika wa maonyesho hayo.

Jephline, aidha, hukuza njugu karanga, mboga za kienyeji kama vile mchicha (almaarufu terere) na mihogo Rongo, Kaunti ya Migori na anataja mimea asilia kama mbinu bora zaidi kuangazia kero ya njaa na uhaba wa chakula nchini.

“Chini ya Rongo Livelihood Women Group, tumefanikiwa kulisha familia zetu na hata kujipa mapato,” akaambia Akilimali kupitia mahojiano ya kipekee.

Kundi hilo la kina mama 22 lililoanzishwa 2018, linaendeshwa chini ya Community Mobilization Against Desertification.

Huku shabaha nyingine ikiwa kuangazia masuala ya afya, vilevile, huongeza mazao thamani haswa njugu kwa kuunda siagi na Jephline anakiri hatua hiyo ina faida tele.

Siagi ambayo Jephline Ojwan’g amesindika kwa kutumia njugu karanga. PICHA|SAMMY WAWERU

Florence Mutugi, mkulima kutoka Kaunti ya Kirinyaga alishiriki maonyesho hayo, meza yake na wanachama wenza wa Neema Farmers Community Garden ikisheheni aina mbalimbali ya maharagwe na mbegu za mboga asilia kama vile murenda, managu, saga na terere.

Cha kufurahisha zaidi, ni maharagwe ya zamani yaliyopamba jukwaa la kundi hilo, mfano, yale meupe yenye virutubisho anuwai yayojulikana kama ‘noe’ katika jamii ya Agikuyu.

Florence Mutugi (kulia), mkulima kutoka Kaunti ya Kirinyaga na mwanachama mwenza wa Neema Farmers Community Garden wakichambua maharagwe ya kutambaa. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tuliungana 2019, wengi wetu tukiwa kina mama kurejesha kwa kuzalisha nafaka asilia. Maharagwe kama vile noe, yana virutubisho vingi vya Protini, ambayo kando na kutufaa kimapato, tunanufaika kiafya,” Florence akaelezea, akibainisha hatua kimaendeleo walizopiga.

Mwavuli wa ISFAA unaoshirikisha Makavazi ya Kitaifa – Kenya, Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi, Taasisi ya Utafiti wa Maliasili za Jenetiki (GERRI), Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), Mtandao wa Kulinda Mbegu (SSN), Biovision Africa Trust (BVAT), Wakfu wa Heinrich Boell (HBF), Consumer Grassroots Association(CGA), miongoni mwa mashirika na kampuni zingine, kupitia hafla hiyo ulisaidia kuleta pamoja wakulima, walaji na asasi mbalimbali za serikali na kibanafsi katika kilimo.

Wanafunzi wa taasisi kadha za masuala ya kilimo na afya, pia walihudhuria.

Mojawapo ya maharagwe yanayoweza kutumika kuzuia uvukizi, kwekwe kumea na mmomonyoko wa udongo shambani. PICHA|SAMMY WAWERU

Anglican Development Services (ADS), kutoka Magharibi mwa Kenya, ilivumisha manufaa ya ukuzaji wa mbegu zinazoorodheshwa kwenye familia ya Legumi kusaidia kukabiliana na kero ya kwekwe, kuzuia uvukuzi na kuongeza Nitrojini udongoni.

“Tunashirikiana na makundi ya wakulima kuhamasisha teknolojia na bunifu katika kilimo kukwepa kero ya tabianchi. Maharagwe kama vile mucuna, soya, dolicopes yanakua haraka na kuongeza rutuba udongoni.

“Nafaka zingine ni njugu, njugu aina ya bambara na seam seam, na kimsingi maharagwe yote yanasaidia kuzuia uvukizi, kwekwe kumea, na mmomonyoko wa udongo, hivyo basi yanaweza kupandwa kati ya mimea mingine,” Florence Omutimba, Mratibu wa Mradi akafafanua.

Florence Omutimba, Mratibu wa Mradi ADS – Western akielezea mkulima kuhusu ukuzaji wa nafaka asilia. PICHA|SAMMY WAWERU

ADS – Western, shirika la kimishonari, lilianzishwa 1997 na muungano wa makanisa ya Kianglikana eneo la Magharibi mwa Kenya likiwa na malengo ya kuangazia usalama wa chakula na lishe, afya na ulinzi wa kijamii, utawala na ushawishi, na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Karen Nekesa, mwanachama wa ISFAA, alisema maonyesho hayo ni hafla ya kila mwaka kuhamasisha wakulima na wananchi haja ya kurejelea mazao na chakula asilia.

Mwanachama wa ISFAA akionyesha boga (lenge) asilia. PICHA|SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Rapudo athibitisha kutengana na Amber Ray akilaumu...

Kamati ya Seneti yajitetea ikisema haikudandia pesa za...

T L