• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kiganjo Kings inalenga kupanda ngazi msimu huu

Kiganjo Kings inalenga kupanda ngazi msimu huu

NA JOHN KIMWERE

LICHA ya kuwa Kiganjo Kings FC inapitia changamoto nyingi za kifedha, ni miongoni mwa vikosi vinavyolenga kupambana mwanzo mwisho, vikilenga kufuzu kushiriki soka ya Ligi Kuu ya Kenya ndani ya miaka mitano ijayo.

Aidha Kiganjo Kings FC ni kati ya timu 17 zinazoshiriki soka ya kuwania ubingwa wa kipute cha Central Regional League (CRB) muhula huu.

Pia Kiganjo Kings ni miongoni mwa timu zinazofanya vizuri kwenye kampeni hizo msimu huu kinyume na ilivyokuwa mwaka 2021.

”Sina shaka kwa sababu mwaka huu tumekaa vizuri kubeba tiketi ya kusonga mbele endapo tutaendeleza mtindo wa kushinda mechi zijazo,” mwenyekiti wa klabu hiyo, Stephen Marubu alisema na kuongeza kuwa kipute hicho bado kinashuhudia upinzani mkali.

Kadhalika anasema wamepania kumaliza kidedea na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi muhula huu.

Mwenyekiti huyo anashikilia kuwa ukosefu wa ufadhili ni kati ya pandashuka ambazo huchangia klabu nyingi kutofanya vizuri na kufanya wachezaji wengi kutotimiza malengo ya kuibuka wachana nyavu wa kimataifa.

Anatoa wito kwa wahisani wajitokeze popote walipo ili kuungana nao kwenye jitihada za kukuza talanta za wapiga gozi wanaokuja. Hata hivyo anashukuru wachezaji kwa kuonyesha mchezo mzuri kwenye kipute hicho wanachoshiriki kwa mara ya pili.

”Bila kuongeza kachumbari tunaona tunaendelea vyema lakini hatuwezi kujigamba kuwa eti tayari tumefanya kweli kwa sababu bado tuna kibarua kigumu mbele yetu,” meneja wake, Samuel Kiarie alisema na kuongeza wanazidi kupiga hatua kwenye kampeni za muhula huu.

Anashikilia kuwa wanayo nafasi ya kufanya vizuri endapo wataendeleza mtindo wa kushinda mechi zao.

Anasema kuwa jambo linalowapiga breki ni ukosefu wa ufadhili lakini watajizatiti kadiri ya uwezo wao kubakili wapinzani wao kwenye mechi zijazo.

Akiri kuwa vipo vikosi kadhaa ikiwamo CMS Allstars, Gatongora FC, Kiambu Community, Sporty na Shamako miongoni mwa vingine vinavyowakosesha usingizi kwenye kampeni zao.

Licha ya kuzabwa mabao 2-1 na Sporty FC wiki iliyopita, meneja huyo anasema, ”Kusema ukweli hatukutarajia kama tungepoteza mechi hiyo lakini ndio hivyo tuliteleza na tuna imani tufanya vizuri kwenye mechi zijazo.”

Kwenye msimamo wa ngarambe hiyo, Kiganjo Kings inashikilia nafasi ya pili kwa kuzoa 25, sawa na Gatongora FC tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kushiriki mechi 13 na 14 mtawalia. CMS inaongoza kwa kuzoa alama 30 baada ya kushiriki mechi 14.

Mwenyekiti huyo anatoa wito kwa wachezaji wake kamwe kutolaza damu dimbani.

Anawahimiza kuwa wanaposhiriki mechi zao nyakati wawe makini zaidi huku kusudi lao likiwa kuvuna alama zote muhimu ili kutimiza azma yao msimu huu.

 

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mahiri na mshairi stadi

Arsenal wakomoa West Ham United ugenini na kurejea nne-bora...

T L