• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kivumbi 2022 marafiki wakipimana nguvu

Kivumbi 2022 marafiki wakipimana nguvu

Na LEONARD ONYANGO

MASHINDANO ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, yamefanya wanasiasa waliokuwa wandani zamani, kugeuka maadui huku kampeni kuelekea Agosti 9 zikipamba moto nchini.

Wanasiasa wamekuwa wakirushiana cheche za maneno licha ya kuunga mwaniaji sawa wa urais.Katika Kaunti ya Siaya, Seneta James Orengo na Gavana Cornel Rasanga, wamegeuka mahasimu licha ya kushirikiana katika uchaguzi wa 2017.

Gavana Rasanga anakamilisha muhula wake wa mwisho mwaka ujao, na ametangaza azma ya kuwania ubunge wa Alego Usonga.Bw Orengo ambaye sasa analenga kuwania ugavana wa Siaya katika Uchaguzi Mkuu ujao, hata hivyo, anaunga mkono mbunge wa sasa wa Alego Usonga, Bw Samuel Atandi.Bw Orengo anataka Bw Rasanga aende kumsaidia kinara wa ODM Raila Odinga kusaka kura za urais kote.

Seneta wa Kisii, Prof Sam Ongeri na mbunge wa Nyaribari Masaba, Bw Ezekiel Machogu – ambao wote wametangaza kuwania ugavana wa Kisii – sasa ni maadui wa kisiasa licha ya kuwa na uhusiano wa kifamilia.

Katika Kaunti ya Homa Bay, Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi na Mwakilishi wa Wanawake Gladys Wanga, wametofautiana vikali licha ya wote kuwa wafuasi sugu wa Bw Odinga.Bw Mbadi amekuwa akitumia mikutano yake ya kisiasa kumshambulia Bi Wanga akidai alifuja mamilioni ya fedha za NGAAF ambazo Waakilishi wa Kike Kaunti hutengewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kaunti zao.

Mwezi uliopita, wafuasi wa Bw Mbadi na Bi Wanga walipigana wakati wa hafla ya kuchangisha fedha katika Shule ya Upili ya Wayara, eneobunge la Ndhiwa. Magari mawili ya Bw Mbadi yaliharibiwa wakati wa ghasia hizo.

Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o na Seneta Fred Outa, walikuwa katika mrengo mmoja katika uchaguzi wa 2017, lakini sasa wamegeuka maadui wa kisiasa.Bw Outa ametangaza azma yake ya kuwania ugavana wa Kisumu kupitia tiketi ya chama cha ODM.

Hata hivyo, mwaka jana, Bw Odinga alionekana kuidhinisha Prof Nyong’o aliposema kiongozi huyo ‘amefanya kazi nzuri’ na anastahili miaka mingine mitano.Bw Odinga amewarai watakaokosa tiketi ya ODM kutohama chamani. “Ukikosa tiketi ya ODM usihame chama.Usipopata tiketi salia chamani kazi ni nyingi serikalini nitawapa nikiingia Ikulu,” akasema Bw Odinga alipokuwa akizungumza katika eneo la Likoni, Mombasa, wiki iliyopita.

Katika kambi ya Naibu wa Rais William Ruto, wandani wake; Gavana wa Nandi Stephen Sang na Seneta Samson Cherargei wanapapurana mara kwa mara hadharani.Bw Cherargei ambaye ni mtetezi mkuu wa Dkt Ruto, analenga kumpokonya Bw Sang wadhifa huo 2022.

Bw Cherargei na Bw Sang’ waliungana 2017, kumng’oa gavana wa kwanza wa Nandi, Dkt Cleophas Lagat.Pia mvutano mkali umeibuka baina ya mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na Bw Caleb Kositany kuhusiana na kiti cha ugavana wa Kaunti ya Uasin Gishu.Bw Kositany ametangaza kuwania ugavana wa Uasin Gishu. Lakini Bw Sudi anapigania Naibu Gavana wa Uasin Gishu Daniel Chemnor awe mrithi wa Gavana Jackson Mandago.

Aliyekuwa Katibu wa Mipango Irungu Nyakera na Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Bi Sabina Chege, wamekuwa wakirushiana cheche za maneno wote wakilenga kumrithi Gavana Mwangi wa Iria.Naye Gavana wa Kiambu, Dkt James Nyoro na Seneta Kimani wa Matangi, wamekuwa wakivutana kwa miezi kadhaa.

Seneta Wamatangi ametangaza azma yake ya kuwania ugavana.Vile vile, Kiongozi wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula ametangaza kuunga mkono Spika wa Seneti Ken Lusaka katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Bungoma mwaka ujao. Msimamo huo umezua uhasama mkubwa kati yake na Gavana Wycliffe Wangamati ambaye ndiye gavana pekee wa chama cha Ford Kenya.

You can share this post!

Polisi walia mishahara yao kupunguzwa

Himizo Lusaka aache ugavana na kulenga juu zaidi

T L