• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Krop na Jebitok wang’ara mbio za nyika za Kapsokwony

Krop na Jebitok wang’ara mbio za nyika za Kapsokwony

Na BERNARD ROTICH

Jacob Krop na Edinah Jebitok waliibuka mabingwa wa duru ya nne ya mbio za nyika za Shirikisho la Riadha Kenya (AK) katika eneo la Kapsokwony kwenye Mlima Elgon, kaunti ya Bungoma, Jumamosi.

Krop aliongoza kitengo chake cha kilomita 10 kutoka mwanzo hadi mwisho na kukata utepe kwa dakika 30:26.81. Alifuatiwa kwa karibu na Samwel Kibet (31:03.35) na Reuben Longosiwa (31:19.70).Krop alisema lengo lake kubwa ni kupata tiketi ya kushiriki duru ya dunia ya Mbio za Nyika ya Agnes Tirop katika kaunti ya Uasin Gishu mnamo Februari 12, 2022.

Jebitok alitawala mbio za kinadada kwa dakika 34:01.91 akifuatiwa na Nelly Cheptoo (35:16.59) na Alice Aprot (35:41.10). Mwanafunzi wa kidato cha pili kutoka Shule ya Chepton katika kaunti ya Nandi, Jebitok alifurahishwa na ushindi wake akisema anashiriki mbio za nyika ili kujinoa kwa msimu wa mbio za uwanjani. Jebitok pia analenga kushiriki Mbio za Nyika za Agnes Tirop mwezi Februari pamoja na Riadha za Dunia mjini Oregon, Eugene nchini Amerika.

Katika mbio za chipukizi za wanaume za kilomita nane, Brian Kiptoo aliibuka mshindi kwa dakika 24:57.40. Alifuatwa kwa karibu na Dismas Yego (25:09.73) na Timothy Kibet (25:18.49). Edna Chepkemoi alishinda mbio za kinadada chipukizi za kilomita sita kwa dakika 21:05.85 akifuatiwa na Deborah Chemtai (1:13.26) na Grace Lolbach (21:32.96).

Duru ya mwisho ya Mbio za Nyika za AK itaandaliwa Desemba 5 katika eneo la Sotik katika kaunti ya Bomet.

You can share this post!

Soi na Chepchirchir watwaa mataji ya La Rochelle Marathon...

PAA sasa kuwika kote ikijitafutia umaarufu kisiasa

T L