• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
‘Matilda Sakwa arejeshwe awe Mkurugenzi Mkuu wa NYS’

‘Matilda Sakwa arejeshwe awe Mkurugenzi Mkuu wa NYS’

NA CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge kutoka eneo la Magharibi mnamo Alhamisi, Aprili 13, 2023 walimshutumu Waziri wa Utumishi wa Umma, Jinsia na Vijana Aisha Jumwa kwa kuhamisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS) Matilda Sakwa kutoka wadhifa huo hadi idara nyingine.

Wakiongozwa na Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, na wabunge Cathrine Amayo na Jack Wamboka walisema kitendo hicho ni kielelezo cha chuki ya kikabila inayoendelezwa na Serikali ya Kenya Kwanza.

Aidha, viongozi hao walisema kuwa hatua hiyo ya waziri Jumwa inaonyesha ubaguzi wa kijinsia “ikingatiwa kuwa Bi Sakwa amefanya kazi nzuri zaidi katika NYS tangu alipoteuliwa  mnamo 2018.”

“Kwetu hii kitendo cha kushushwa cheo kwa Mkurugenzi wa NYS Bi Matilda Pamela Sakwa ni kitendo cha ubaguzi wa kijinsia na chuki ya kikabila. Mtumishi huyo wa umma ameshushwa cheo sio kwa sababu ya utendakazi mbaya bali ni kwa sababu yeye ni mwanamke kutoka jamii ya Waluhya,” akasema Bw Amisi ambaye ni Mbunge wa Chama cha ODM.

“Kwa hivyo, kwa niaba ya jamii ya Waluhya na raia wa nchini, tunawasilishwa matakwa yafuatayo; Kwamba Mkurugenzi wa NYS Bi Matilda Pamela Sakwa arejeshewe wadhifa wake. Aidha, tunataka mageuzi yafanywe katika utumishi wa umma ili kulinda kazi za watumishi wa umma ambao hawatoki makabila ya Kalenjin na Kikuyu. Isitoshe, tunatoa wito kwa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuchunguzi visa vya maonevu na ubaguzi katika utumishi wa umma,” wabunge hao wakasema.

Kwa upande wake seneta Osotsi alidai, bila kutoa ushahidi, kwamba Bi Sakwa alishushwa hadhi na waziri Jumwa kwa sababu alikataa kutoa zabuni kwa wakuu fulani wa serikali ya Kenya Kwanza kinyume cha sheria.

“Bi Sakwa alikataa agizo hilo kwa sababu hakutaka sakata nyingine kuchipuka katika NYS baada ya ile sakata ya mwaka wa 2015 ambapo Sh760 milioni ziliporwa,” akasema.

Bw Amayo alishutumu Waziri Jumwa kwa kumshusha cheo Bi Sakwa ilhali ni mtumishi wa umma aliyehitimu barabara kwa kazi hiyo.

“Tunajua kwamba ni Waziri Jumwa ambaye alikuwa na wakati mgumu kuelezea kiwango chake cha masomo alipokuwa akihojiwa kwa uteuzi kuwa Waziri. Sasa mbona anamdhulumu Bi Sakwa, ambaye amehitimu sawasawa kwa kufanya kazi nzuri ya kuleta mageuzi katika NYS?” Mwakilishi huyo Wanawake, Kaunti ya Busia akauliza.

Bi Sakwa aliteuliwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo 2018 alipokuwa akihudumu kama Kamishna wa Kaunti ya Machakos.

Bi Sakwa alichukuwa nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa NYS kutoka kwa James Tembur ambaye alikuwa ameshikilia wadhifa huo kama kaimu kwa muda wa mwezi mmoja.

Awali, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai na naibu wake Sam Michuki waliondolewa afisini baada ya kushtakiwa kuhusiana na kupotea kwa Sh469 milioni.

Bw Ndubai alichukua hatamu kutoka Nelson Githinji ambaye alisumwa kortini kutokana na sakata ya wizi wa Sh760 milioni katika NYS.

Bi Sakwa ni afisa wa utawala wa miaka mingi ambaye wakati huu anasomea shahada ya uzamifu.

Amehitimu kwa shahada ya uzamili katika kozi ya elimu ya maendeleo kutoka Taasisi ya Kimataifa kuhusu Masomo ya Kijamii, katika Chuo Kikuu cha Erasmus Rotterdam nchini Uholanzi.

  • Tags

You can share this post!

Waendesha pikipiki wa Kenya watupia jicho mashindano ya...

Ukabila ulivyokolea katika Serikali Kuu

T L