• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Memphis Depay afunga mabao matatu na kuongoza Uholanzi kuponda Uturuki

Memphis Depay afunga mabao matatu na kuongoza Uholanzi kuponda Uturuki

Na MASHIRIKA

MEMPHIS Depay alifunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya kwanza akivalia jezi ya timu ya taifa ya Uholanzi mnamo Jumanne dhidi ya Uturuki katika mechi ya Kundi G kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Davy Klaassen aliwafungulia Uholanzi ukurasa wa mabao katika dakika ya kwanza kabla ya Depay ambaye ni fowadi matata wa Barcelona, kupachika wavuni mabao matatu na kufanya mambo kuwa 4-0 kufikia dakika ya 54.

Guus Til na Donyell Malen walifunga mabao mengine ya Uholanzi waliowateremkia zaidi wageni wao jijini Amsterdam baada ya beki wa Uturuki, Caglar Soyuncu anayechezea Leicester City kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 44.

Depay, 27, sasa amefikia rekodi ya Johan Cruyff na Abe Lenstra ambao wanashikilia nafasi ya nane kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa Uholanzi baada ya kujivunia mabao 33 kapuni mwake.

Mfumaji huyo wa zamani wa Olympique Lyon na Manchester United amefunga mabao 12 kutokana na mechi 10 zilizopita za kimataifa, yakiwemo mawili katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na Uholanzi dhidi ya Montenegro mnamo Septemba 4, 2021.

Uturuki ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kundini kwa alama 11, walifutiwa machozi na Cengiz Under katika dakika ya 90.

Uholanzi wanaotiwa makali na kocha Louis van Gaal sasa wamefunga mabao 16 kutokana na mechi sita na wanadhibiti kilele cha Kundi G kwa alama 13 sawa na Norway.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Griezmann abeba Ufaransa dhidi ya Finland

Haaland hachoki kufunga, amepachika wavuni mabao 11...