• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Tathmini ya hadithi ‘Mwalimu Mstaafu’

Tathmini ya hadithi ‘Mwalimu Mstaafu’

MWALIMU Mstaafu ni hadithi katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba iliyoandikwa na Dumu Kayanda.

Tutaichambua hadithi hii kwa kuzingatia vigezo kadha:

WAHUSIKA

i) Mwalimu Mosi

(ii) Jairo

iii) Mkewe Jairo

(iv) Wanafunzi

(v) Wanawe Jairo – Sabina

(vi) Bi Sera – mkewe Mwalimu

MANDHARI

i) Shuleni

ii) Nyumbani kwa mwalimu

MTIRIRIKO

Mwalimu Mstaafu aliandaliwa sherehe ya kumuaga shuleni wakati wake wa kustaafu ulipotimu. Wanafunzi wake wa zamani waliungana na waliokuwa kumzawidi mwalimu wao aliyechangia makuzi yao.

Aliposimama kuhutubu, alisisitiza hata wale waliokuwa na maoni tofauti, si kusifu tu, pia wapewe muda kuzungumza. Jairo alijitokeza. Alimlaumu mwalimu kwa kumharibia wakati kwa kumpa maarifa ambayo hayajamfaidi maishani.

Watu walimpa mwalimu zawadi kemkem. Akaagiza zawadi zile zipelekwe kwake Jairo. Jairo alienda kulalamikia kuaibishwa na mwalimu kwa kumkabidhi zawadi zile. Alijibu kwa kumpa mkewe na wanawe kama zawadi.

Mkewe Jairo na Bi Sera waliingiliana. Watoto wake wakapelekwa shuleni. Sabina alisajiliwa katika shule ya bweni. Uvumi ukaenezwa kijijini kuwa Mwalimu alimpangia Sabina chumba mjini na kuwa mpenzi wake. Uvumi huu ulimfikia Jairo, aliyeenda kumkabili Mwalimu kwake. Ukweli unapobainika, anaomba msamaha kwa kumuumbua Mwalimu. Soni inamvaa na kumsukuma kuthubutu kujitoa uhai. Wanakijiji wanamnusuru.

DHAMIRA

Hadithi inaangazia umuhimu wa kuwajibika. Mwalimu anastahiwa na jamii kwa kuifanya kazi yake kwa uaminifu. Hadithi pia imeangazia umuhimu wa elimu maishani. Walioelimika hupata nafasi ya kuishi maisha ya fahari. Wanafunzi wa mwalimu wanawasili kwa magari ya kifahari, wamevalia nguo za bei ghali, ishara tosha ya ufanisi wao.

MAUDHUI

Uwajibikaji

i) Wanaowajibika maishani hupata ufanisi. Mwalimu alifanya kazi yake kwa moyo mmoja. Aliwapa wanafunzi mafunzo ya darasani na kuwanasihi. Wazazi kwa wanafunzi wanafika kutoa shukrani zao.

ii) Wanafunzi waliofuata mafunzo yake mwalimu waliwajibika na kuvuna matunda ya bidii zao. Hatimaye waliishia kuwa watu wa kutajika maishani; madaktari, marubani, wahandisi na wahasibu.

iii) Wanafunzi waliotelekeza jukumu lao la kufuata maagizo ya walimu waliishia kuwa watu wasiothaminiwa katika jamii. Jairo anawakilisha kikundi hiki. Anaamini hakuumbiwa shule, na mwalimu alimpotezea wakati. Inaashiria hakutia bidii masomoni, ndiyo sababu hakuambulia chochote. Anakiri wanajamii wamempuuza, hajawahi kuitwa ‘mtu wa maana’. Anaishia kuwa mlevi, hali inayomzuia kuchangia maendeleo katika jamii.

iv) Jairo ametelekeza jukumu lake la kuwa mlezi wa jamii yake. Baada ya kuwapeleka familia kwa mwalimu, hafuatilii maisha yao. Wazushi wanapomwambia Mwalimu amemgeuza Sabina kuwa mpenzi wake, anaamini kwani hachunguzi ukweli wa mambo. Anapoelewa ukweli, anaaibika kwani wanawe wametunzwa vilivyo.

Uchambuzi huu utaendelea wiki ijayo.

Grace Ogoye

Kisumu Girls High School

You can share this post!

TAMTHILIA: Maendelezo ya Onyesho la Tatu, Tendo la Kwanza...

Hofu ardhi ya ekari 9,000 imenyakuliwa

T L