• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 1:50 PM
MWALIMU WA WIKI: Analenga kuwa profesa karibuni

MWALIMU WA WIKI: Analenga kuwa profesa karibuni

Na CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya kuongoza wanafunzi kufikia malengo yao ya kiakademia, mwalimu bora anapaswa pia kuwa mlezi wa vipaji vya watoto, rafiki wa karibu na mshauri wao kuhusu masuala mbalimbali maishani.

Mwalimu anayejali maslahi ya wanafunzi anastahili kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya somo lake. Ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote na asome kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Margaret Njogu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya Magomano Girls, Kaunti ya Nyandarua.

“Mwalimu anastahili kuwa kielelezo chema kwa wanafunzi. Awahimize mara kwa mara katika safari ya elimu, atambue changamoto wanazozipitia, aelewe udhaifu na kiwango cha mahitaji ya kila mmoja wao na awaamshie hamu ya kuchapukia masomo,” anasema.

Margaret alilelewa katika eneo la Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga. Ndiye wa saba kuzaliwa katika familia ya watoto 10 wa Bw Joseph Ngiri na Bi Teresiah Nyawira.

Alisomea katika shule ya msingi ya Kiamaina, Kagumo hadi 1993 kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Kiburia Girls iliyoko Gichugu, Kirinyaga (1994-1997).

Alisomea ualimu (Kiswahili/Muziki) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kati ya 1999 na 2003.

Uamuzi wake wa kujibwaga katika ulingo wa ualimu ulikuwa zao la kuchochewa zaidi na Bw Kabugua na Bi Warui waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi na upili mtawalia.

Kabla ya kufuzu chuoni, Margaret alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Kiburia mnamo 2003. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Aliwahi pia kufundisha katika shule ya St Philip’s, Embu (2003-2004) kabla ya kuhamia shule ya Ngorika, Nyandarua (2005-2007) kisha St Anuarite Girls iliyoko Njabini, Nyandarua (2007-2008).

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri 2008 na kumtuma kufundisha katika shule ya Karoti Girls, Kirinyaga. Alihudumu huko kwa miaka sita kabla ya kuhamia Magomano Girls mnamo 2014.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Ushauri Nasaha mnamo 2017 kabla ya kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Margaret aliwahi kuwa Kaimu Naibu wa Mwalimu Mkuu wa Magomano Girls kuanzia 2021 hadi Juni 2022.

Mbali na ualimu, Margaret ni mshairi shupavu na mwanafasihi chipukizi. Anajivunia kuchapishiwa ‘Mwongozo wa Tamthilia ya Kifo Kisimani’ (Kithaka wa Mberia) mnamo 2009 na sasa ana mswada wa diwani ya mashairi uliopo katika hatua za mwishomwisho za uhariri.

Tangu 2014, Margaret amekuwa mstari wa mbele kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti kwenye tamasha za kitaifa za muziki (KMF).

Shairi lake ‘Anasa’ lililokaririwa na wanafunzi wa Magomano Girls katika KMF 2018 liliambulia nafasi ya tatu kitaifa.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Margaret ni kujiendeleza kitaaluma na kuweka hai ndoto za kuwa mwalimu mkuu kisha profesa wa Kiswahili na mhadhiri wa chuo kikuu. Anapania pia kuzamia kikamilifu katika uandishi wa fasihi ili kuendeleza kipaji cha utunzi wa kazi bunilizi kilichoanza kujikuza ndani yake utotoni.

Kwa pamoja na mumewe Bw Isaac Njogu, wamejaliwa watoto watatu. Bw Njogu kwa sasa ni mwalimu wa masomo ya Hisabati na Biashara katika shule moja ya upili iliyoko Nyandarua.

  • Tags

You can share this post!

Mke wa Naibu Rais aahidi kuhakikisha shule ya Mugumoini...

TAHARIRI: Wabunge wasitishe ulafi, wajali waathiriwa wa...

T L